Header Ads

Umeme wa Gridi kuokoa bilioni 30 kwa mwaka Njombe, Ruvuma


Na Greyson Mwase, Ruvuma
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa mara baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa umeme utakaopelekea mikoa ya Njombe na Ruvuma kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa Septemba, 20 mwaka huu, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) litaweza kuokoa shilingi bilioni 30 zilizokuwa zikitumika kama gharama ya kuendesha mitambo ya kuzalishia umeme inayotumia mafuta mazito katika mikoa hiyo.
Waziri Kalemani aliyasema hayo mapema jana tarehe 04 Juni, 2018 kwa nyakati tofauti kupitia mikutano na vijiji vya Suluti kilichopo wilayani Namtumbo na Lukumbule na Mkowela vilivyopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma kwenye ziara yake ya kukagua njia ya Makambako – Songea, vijiji vinavyotakiwa kuunganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa pamoja na miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Katika ziara hiyo Waziri Kalemani aliambatana na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakandarasi pamoja na wakuu wa wilaya husika.
Dkt. Kalemani alisema kuwa, shirika la Tanesco limekuwa likitumia gharama kubwa ya shilingi bilioni 30 kwa mwaka kama  gharama ya uendeshaji wa mitambo inayotumia mafuta mazito katika mikoa ya Njombe na Ruvuma na kusababisha hasara badala ya faida.
Alisema kuwa, mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Makambako, Madaba na Songea mapema mwezi Septemba mikoa ya Njombe na Ruvuma itaunganishwa rasmi na Gridi ya Taifa na kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 30 kinachotumika kuendesha mitambo ya mafuta mazito gharama ambazo ni kubwa tofauti na mapato ya shirika hilo ya shilingi bilioni tisa kwa mwaka kwa mikoa husika.
Aidha, aliongeza kuwa kuingizwa katika Gridi ya Taifa kwa mikoa ya Njombe na Ruvuma kutapelekea uwepo wa nishati ya uhakika na kuchochea ukuaji wa uchumi.
 Kazi ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Songea kilichopo mkoani Ruvuma ikiendelea.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kulia) akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara yake katika kituo cha kupoza umeme cha Songea kilichopo mkoani Ruvuma. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema na kushoto ni Msimamizi wa Mradi wa Umeme wa Makambako – Songea, Mhandisi Didas Lyamuya.
 Sehemu ya wananchi wa kijiji cha  Suluti kilichopo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) alipokuwa akiwaelezea mikakati ya serikali katika upelekaji wa huduma ya umeme vijijini.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akielezea matumizi ya kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kwa wananchi wa kijiji cha  Suluti kilichopo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma (hawapo pichani)
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akielezea mikakati ya Wizara ya Nishati kwenye usambazaji wa miundombinu ya umeme katika mikoa ya Njombe na Ruvuma katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Omela.

No comments:

Powered by Blogger.