MSD YAKARABATI JENGO LA DUKA LA DAWA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI KWA KASI KUBWA KUTEKELEZA AGIZO LA RAIS DK.MAGUFULI
Mafundi wakikarabati jengo ambalo Bohari
ya Dawa (MSD), itafungua duka la dawa katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MSD) Dar es Salaam jana kwa ajili ya kuhudumia wananchi kwa
karibu zaidi vikiwemo vifaa tiba. Duka hilo linatarajiwa kufunguliwa
kesho kutwa.
Fundi akitoboa ukuta sehemu litakapo fungwa beseni la kunawia katika duka hilo.
Mafundi wakiendelea na ukarabati wa jengo hilo lililopo jirani na wodi ya Kibasila linalotizamana na maegesho ya magari.
Fundi akipaka rangi ndani ya jengo hilo.
Jengo la duka hilo la MSD linavyoonekana kwa nje. Hapa mafundi wakiendelea na kazi ya ukarabati.
Na Dotto Mwaibale
BOHARI ya Dawa (MSD) imejiimarisha na
kuhahikisha inatekeleza kwa wakati agizo la Rais Dk. John Magufuli la
kuweka maduka ya dawa katika hospitali za rufaa na kanda nchini.
Katika kutekeleza agizo hilo MSD imeanza
kwa kasi kubwa ya kukarabati jengo la duka la dawa katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili (MNH), ambalo linatarajiwa kufunguliwa kesho.
Mwandishi wa habari hii alishuhudia jana
kasi kubwa ya mafundi ujenzi wakikarabati jengo hilo ambalo awali
lilikuwa likitumika kama stoo ya kuhifadhi vitu mbalimbali vya hospitali
hiyo.
Akizungumza na vyombo vya habari hivi
karibuni kuhusu ufunguzi wa maduka hayo, Mkurugenzi Mkuu wa MSD,
Laureane Bwanakunu alisema agizo la Rais la kuitaka MSD kuanzisha duka
la dawa karibu na hospitali limekuja wakati muafaka kwani kwenye mpango
mkakati wa miaka sita wa MSD tayari ilikuwa na mpango wa kufungua
maduka hayo kwa ajili ya kusogeza huduma karibu a wananchi.
Alisema maduka ya MSD ambayo
yatafunguliwa kwenye hospitali za rufaa na kanda yatafanya kazi masaa 24
na kuuza dawa na vifaa tiba chini ya bei ya soko pia yatahudumia watu
binafsi na wale waliopo kwenye taratibu za Bima ya afya kote nchini.
"Ili kudhibiti watumishi wasio waaminifu
kuiba dawa MSD inafanya kazi za uagizaji, uhifadhi na usambazaji kwa
kutumia mfumo wa mtandao wa E9 na tangu mwaka wa fedha uliopita tumeanza
kuziwekea alama ya GOT bidhaa zetu ikiwa ni pamoja na vidonge." alisema
Bwanakunu.
Alisema vidonge ambavyo tayari
vimewekewa nembo ya GOT vipo 45 na wanaendelea kuwapa maelekezo wazabuni
ili vyote viwekwe alama hizo..,nembo ya serikali inaonekana kwenye dawa
za serikali kama Diclofenac, moxillin, iprofloxacin,
Contrimoxale,paracetamol,
na magnesium.
Alisema wanatarajia kuanzisha huduma ya
kutoa taarifa kwa njia ya simu pale wananchi watakapoona kuna wizi wa
dawa za serikali na kwamba wananchi wanaelimishwa kutoa taarifa pale
wanapoona dawa za serikali mitaani.
Alisema, pamoja na serikali kuanza kupunguza deni lake linalodaiwa na MSD bado inadaiwa Sh.bilioni 53.
|
|
|
No comments:
Post a Comment