MGODI UNAOTEMBEA: Chadema kinakufa huku kinacheka
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam.
NI
dhahiri Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kinakufa huku
kinacheka. Kuisema kauli hii kwa Tanzania ya leo, kunahitaji moyo wa
chuma. Baadhi ya watu wasiopenda kukoselewa au kuelekezwa jambo wataanza kupayuka. Watapaza sauti zao juu kupinga kila wawezalo.
Ila
mwisho wa siku ukweli utadhihiri, maana wahenga wana msemo wao kuwa
siku zote majuto ni mjukuu. Kauli hii inatufundisha watu kujifunza vitu
kabla ya kuingia kwenye mihangaiko ya moyo. Naitamka kauli hii kwa kuangalia jinsi watu wanavyotaka kuyumbisha mambo na kufikia kuogopa baadhi ya sura ndani ya Chadema.
Kuogopwa
kwa watu hao ni kwa Mwenyekiti wake Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake
Dk Willbroad Slaa, moja ya watu waliokuwa wakiheshimika na bado baadhi
wanamuheshimu hapa nchini. Ukiwa
wewe ni kiongozi mdogo upo ndani ya Chadema, utasumbuliwa au hata
kuwekwa kando kama utajaribu kukosoa utendaji wa Mbowe na Slaa.
Haya
ni matatizo makubwa. Yanahitaji kuangaliwa upya, ili kesho wasijitokeze
wale wanaosema ushindi wao umechakachuliwa na Chama Cha Mapinduzi
(CCM). Wafuasi hao, itabidi waamini kuwa wameshindwa kutokana na mipango
na dhamira ya kweli ya kuwaongoza Watanzania.
Chadema sasa kumesheheni makundi. Tena makundi ambayo kwa kiasi kikubwa yanaathiri mfumo mzima wa kiutendaji. Japo
wanasiasa wenyewe wanakubali kuwa makundi hayaepukiki, lakini kwa chama
kama Chadema, kinahitaji makundi yenye kujenga kwanza.
Wasipojijenga,
hata malengo ya kuongoza Dola ni mtihani mzito kwao. Licha ya Chadema
kutembea na sera ya kupinga ufisadi, ila ni wazi ndani yao kumesheheni
vitendo vya kidhalimu.
Na
kwakuwa ufisadi ni jambo pana, basi hapana shaka nao wapo miongoni mwa
mafisadi. Ufisadi si kula mali za umma. Ufisadi si kuiba fedha za
serikali tu, ila mahala popote panapojumuisha watu wengi. Leo Chadema wapo watu wanaohitaji wakalie nafasi zao miaka kadhaa mbele. Si jambo baya, ila pia taratibu lazima zifuatwe.
Ni
aibu kubwa Chadema ambacho ni Chama Kikuu cha Upinzani, kushindwa
kujenga hata ofisi zao zinazokwenda sambamba na uhai wao, licha ya
kupokea ruzuku zisizopungua Sh Bilioni 9.2 katika kipindi cha kuanzia
mwaka 2009 hadi 2010.
Chadema
ni chama kisichokuwa na mipango ya kujiwekea miradi ya kimaendeleo,
badala yake inasubiria ruzuku, michango ya wanachama wake na bado
inatumika ndivyo sivyo. Chama
kinajiendesha kwa siri siri. Hakuna uwazi wala uwajibikaji. Uwanja wa
kuhoji uhalali wa jambo moja hadi jingine ndani ya viongozi hao ni
mtihani.
Chadema
kwa sasa wanaishi kama samaki, mkubwa anammeza mdogo. Nyuma ya pazia,
wao ndio wanaohubiri utawala bora, sera, mipango na kusimamia maendeleo
ya serikali, wakati wao wenyewe wanashindwa kujiongoza.
Waliokuwa
nje ya uongozi wa Chadema, wafuasi wao wanabaki kudanganywa tu. Tena
watu hao wanaodanganya hujificha katika kivuli cha mageuzi, wakiamini
kila mtu anataka kuona CCM kikiondoka madarakani.
Kwakuwa
baadhi yao wanahitaji kuona CCM kinakuwa pembeni, basi wanaburuzwa
mchana na usiku. Wakiambiwa lolote hupiga makofi. Wanainua vidole viwili
juu. Wanaimba nyimbo mbaya zinazohusu utawala wa CCM na viongozi wao.
Anayejitokeza kuhoji, anaonekana juha, makuhani. Eti ni mamluki wa CCM. Anaitwa mwajiriwa wa CCM.
Vijana
wa leo hasa katika mitandao ya kijamii wanasema buku 7000. Wakimaanisha
wapo watu wanaolipwa ujira wa elfu saba kila wanapoipigania CCM.
Kweli? Kwa mwendo huu sidhani kama CCM inahitaji kuwalipa wafuasi elfu saba ili wahubiri mema yao. Si kweli hata kidogo.
Ingawa
CCM imeasisiwa tangu mwaka 1977, lakini ina historia nzuri na Taifa
letu. Imefanikiwa kuweka utawala bora kiasi cha kukuza vyama vya siasa
vya upinzani, kama vile Chama Cha Wananchi (CUF), NCCR Mageuzi, TLP,
Chadema, UDP, NRA na vinginevyo vyenye sera na mitazamo tofauti.
Watu
walikuwa wakilala barabarani wanaposafiri umbali mrefu, kama vile
Mwanza, Kagera, Tabora, Arusha, Mtwara na kwingineko. Leo hii mikoa
karibia yote inaunganishwa na barabara za lami na kuna mifumo mizuri ya
kiutendaji. Huduma ua umeme na maji inafanyiwa kazi kwa kasi kubwa mno
na pia uhalali wa watu kuihoji serikali yao.
Ni
tofauti na vyama vya upinzani kikiwamo Chadema, kinachoongozwa na Mbowe.
Tangu kianzishwe mwaka 1992, chama hiki ni ngumu mtu kuinua kinywa
chake kuhoji utawala wa Mbowe na maswahiba zake ndani ya Chadema. Na
ndio maana wengi wanaoinua midomo yao, mara kadhaa huishia nje ya
uongozi wa chama hicho, akiwamo Juliana Shonza, Mtela Mwampamba na juzi
Samson Mwigamba.
Hii ni
mifano iliyotokea ndani ya mwaka huu, hasa baada ya watu hao kuhoji
nyendo za viongozi wao. Suala linapopigiwa kelele ni juu ya Mbowe
kuiendesha chama kama chake. Wengine wanasema ni chama cha kindugu.
Wengine wanasema bila kuwa mtu wa Kaskazini huwezi kuwa na nafasi
Chadema.
Na
ukiwa si wa Kaskazini, basi inakulazimu kubaki kimya ili usinyang’anywe
tonge mdomoni. Ni tofauti na CCM. Japo mfumo huo wakati mwingine
haukwepeki, ila bado Mzigua wa Handeni anaweza kuwania nafasi yoyote
ndani ya chama hicho au akashauri nyendo zenye kujenga utawala bora bila
kufanywa lolote.
Ni jambo la kujiuliza, kama serikali ya CCM na viongozi wake wangekuwa hawataki kusemwa au kushauriwa wangapi wangebaki mtaani?
John
Mnyika, Mbunge wa Ubungo ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa Chadema
aliibuka akisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya
Mrisho Kikwete ni dhaifu. Aliainisha vipengele vingi na kuzua maswali
na wasiwasi dhidi ya nyendo za baadhi ya viongozi wa Chadema. Mbunge wa
Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chadema, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ naye akaingia
kwenye rekodi baada ya kumuita Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa ni
‘mpumbavu’.
Wabunge
kama Godbless Lema, Mchungaji Peter Msigwa na wengineo ndani ya Chadema
wamekuwa wakibadilishana kauli za ukakasi dhidi ya serikali ya CCM,
chini ya Kikwete. Wanaachwa kama walivyo. Lakini maneno hay ohayo
wayaseme kwa viongozi wao, Mbowe na Slaa uone watapewa adhabu gani.
Watavuliwa
uongozi. Maana mkuki kwa nguruwe. Hii ni kwasababu hakuna utawala bora
ndani ya vyama vya upinzani, wakiwamo Chadema. Wao wanaishia kuipigia
kelele CCM lakini ndani ya mioyo yao wapo kifedha zaidi. Ni ajabu na
kweli. Ndio hapo tunaposhuhudia msuguano wao ukiwa katika mshike mshike
wa uenyekiti katika Uchaguzi ambao haueleweki utafanyika lini.
Uenyekiti
ambao watu wanahoji jinsi chama cha siasa kisichokuwa na ukomo wa
uongozi ndani ya Katiba yao. Kipengele hicho hakijajadiliwa? Kwanini?
Ama hakuna anayeweza kuwa mwenyekiti zaidi ya Mbowe na Katibu wake Slaa?
Kelele zote zinaelekea kwa Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini
ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, akiambiwa ndio anayeongoza
kambi inayosumbua chama chake.
Inawezekana,
ila kwa sasa hoja ni utawala bora ndani ya Chadema kuwa sifuri. Hoja ni
matumizi mabaya ya ofisi na kodi za wananchi. Hoja ni kwa namna gani
hakuna utaratibu mzuri wa manunuzi ya vitu vya chama chao?
Ndio maana nasema Chadema kinakufa huku kinacheka. Kifo hiki ni kibaya sana. Maana mtu hajui kama mtu wake anakufa.
Akiangalia
kicheko kinavyopamba sura yake, anaona uhai upo. Akija kushtuka, mauti
yamemkuta na wanabadilisha jina, kutoka fulani hadi marehemu fulani.
Je, Chadema wenyewe wanalijua jambo hili? Je, wamejua kama wanakufa
huku wanacheka? Nani atawakomboa kama wenyewe wanatoana roho? Yu wapi
mwenye ujasili wa kumwambia Mbowe anaendesha chama ndivyo sivyo?
Thubutu?
Hata leo, Lema ni swahiba mkubwa wa Mbowe, lakini akiamua kuhoji mwendo
wao mbaya hakika kiti chake kitakuwa kwaheri. Hawezi kusema lolote.
Ataendelea kukaa kwenye msimamo wa mwenyekiti wake akiamini maisha yake
yanakwenda sawa.
Huu ni
wakati wa Watanzania kuwa makini katika kuviangalia vyama hivi vya
siasa, ambavyo baadhi yao havina malengo mazuri na Taifa lao.
Wanachoweza kufanya ni kuwayumbisha Watanzania kwa kusimamia mambo
yenye faida yao, kusimamia migogoro, maandamano kupinga utawala wa
sheria wa serikali, wakati wao wenyewe wanashindwa kujiongoza na
kusimamia ukweli.
Nakutakia Jumatano njema.
Mungu ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment