Header Ads

CCM: ZIARA ZA KINANA ZIMEONYESHA KUZAA MATUNDA

NA BASHIR NKOROMO.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema ziara ambazo zimekuwa zikifanywa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, zimeanza kuzaa matunda hasa upande wa utatuzi wa kero zinazowakabili wananchi.

Hayo yamesemwa leo, Novemba 12, 2013, na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye wakati akitangaza kuanza kwa ziara ya Kinana ya siku 22, katika mikoa ya mikoa ya Ruvuma na Mbeya itakayoanza, Novemba 15, 2013, ambayo ni mwendelezo wa ziara za kuimarisha chama, kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi  ya CCM ya mwaka 2010, kusikiliza kero za wananchi na kushirikiana nao kuzitafutia ufumbuzi.

Nape alisema miongoni mwa mafanikio yanayoonekana kutokea ni mwitikio ulionyeshwa na serikali katika kutekeleza maagizo yaliyotolewa kupitia ziara zilizopita za Kinana, na vikao vya Chama kuhusu kushughulikiwa kwa kero au hoja mbalimbali.

Alisema, baadhi ya kero ambazo zimeshuhudiwa zikichukuliwa hatua na serikali ni pamoja na kufufua viwanda nchini.

Nape alisema baada ya ziara kadhaa za Katibu Mkuu, uchambuzi na vikao kadhaa vya CCM, Chama kiligundua kuwa viwanda vingi vilivyo binafsishwa havifanyi kazi kama ilivyokusudiwa na vingine kufungwa kabisa na kugeuzwamagodauni.

Alisema pamoja na athari kubwa kwa uchumi wa nch, kufungwa na kutofanya vizuri kwa viwanda hivyo kumechangia sana tatizo la ajira kuwa kubwa, hivyo Chama kiliagiza serikali kufanya tathimini ya viwanda vyote vilivyo binafsishwa na hali yake kwasasa na vile visivyofanya kazi kama ilivyokusudiwa vichukuliwe na serikali na kutafuta njia sahihi ya kuvifufua upya.

Nape alisema, baada ya chama kuagiza kupitia ziara za Kinana na vikao vya Chama, serikali imechukua hatua kadhaa katika hili, ikiwemo kufanya tathimini na mapendekezo kadhaa yamewasilishwa na timu iliyoundwa na serikali kwa serikali kwa ajili ya kufanyia uamuzi na kuchukua hatua.

Alisema, CCM inatambua kwamba zipo hatua kadhaa ambazo imechukuliwa na serikali katika jitihada za kufufua viwanda vya kubangua korosho kama sehemu ya utatuzi wa tatizo la soko na zao la korosho na kwamba  na sasa serikali ipo katika hatua kadhaa za kushughulikia viwanda vingine nchini.

Nape alisema, kutokana na mwitikio huo, CCM inaipongeza serikali kwa hatua hizo muhimu za kutekeleza agizo la Chama, ingawa pamoja na pongezi hizo CCM imeitaka serikali ikamilishe kazi hiyo mapema iwezekanavyo ili nchi ifaidike na ufufuaji huo wa viwanda nchini.

No comments:

Powered by Blogger.