Wachina wamsaidia Kigoda kuchimba visima viwili ili kupunguza tatizo la maji wilayani Handeni
Mbunge
wa Handeni Dkt Kigoda akiwapa maelezo wafadhili wake waliochimba visima
viwili virefu kwa thamani ya shilingi milioni 80, kwamba sasa maji
yaliyopo kwenye vioski hivyo vinasaidia wananchi ambao wanachota kwa
ndoo moja sh. 50 badala ya hapo awali kununua sh. 500.
Na Mashaka Mhando,Handeni
MAKALI
ya tatizo la maji katika mji wa Chanika wilayani Handeni, yameanza
kupungua kufuatia kuchimbwa kwa visima virefu vipatavyo 20 katika mji
huo ili kukabiliana na uhaba mkubwa wa maji ambao ulikuwa kero kubwa
hasa kwa akina mama wanaoshindwa kufanya kazi kwa ajili ya kutafuta
maji.
Kupungua
huko kumebainishwa na mmoja ya akina mama Grace Mwinkalo alipozungumza
katika hafla fupi ya Mbunge wa jimbo hilo, Dkt Abdallah Kigoda alipofika
kwenye moja ya kioski cha maji kilichoko soko la zamani mjini hapa,
kuwaonesha wafadhili mradi wa visima viwili walivyofadhili.
Mbunge
wa Handeni na Waziri wa Viwanda, Biashara na masoko Dkt Abdallah Omary
Kigoda akisalimia na wananchi wa jimbo lake alipofika kuwaonesha
wafadhili wake kisima alichochimba eneo la Chanika Soko la zamani.
Injinia
wa maji wa wilaya Injinia Komba, akimweleza mbunge Dkt Kigoda pamoja na
wafadhili wake akiwemo Mwenyekiti wa TCZMR Bw Zhao Daoquan (shoto kwa
Kigoda), namna walivyoweza kuchimba eneo hilo na kupata maji ambayo
yanatumika kwa sasa na wananchi wa Handeni.
Mama
huyo mkazi wa mtaa wa Kwamngumi kata ya Chanika, alisema wanashukuru
makali ya ukosefu wa maji yamepungua kwa kiasi kikubwa kufuatia sasa
mtaa wao huo na mingine kuwepo kwa visima vilivyochimbwa na mbunge
akishirikiana na wafadhili wake kupunguza kero ya maji iliyokuwepo muda
mrefu.
"Mheshimiwa
mbunge na wageni wako, kwa niaba ya akina mama wa Chanika, tunapenda
kushukuru kwako na serikali kwa ujumla kwani sasa makali ya tatizo la
maji katika mji wetu yamepungua kwa kiasi kikubwa, tunashukuru endelea
kufanya jitihada nyingine ili tuweze kupata maji zaidi," alisema
Mwinkalo.
Akizungumza
kumweleza Mwenyekiti wa Muungano wa Wazalishaji Madini wa Tanzania na
China (TCZMR), Zhao Daoquan, mbunge wa jimbo hilo, alisema msaada wa
visima viwili walivyowapa, vimeweza kusaidia kero ya maji iliyopo
wilayani humo iliyosababishwa na wilaya hiyo kuwa na mito ya kudumu
ikiwemo mabwawa.
Alisema zaidi ya visimwa 20 vimechimbwa
katika maeneo mbalimbali ya wilayani humo ambapo sasa wananchi wananunua
ndoo moja ya maji sh. 50 badala ya sh. 500 hadi sh. 1,000 walizokuwa
wakinunua kipindi cha nyuma hatua ambayo ilikuwa ikisababisha kero na
watu wengine kumlaumu yeye ingawa tatizo la maji ni la Kitaifa.
Naye
mwenyekiti wa TCZMR ambaye ni raia wa China waliopo hapa nchini kwenye
migodo ya Mchuchuma na Liganga hapa nchini, alisema wameanza miradi ya
kusaidia maji katika jimbo la Handeni lakini wataendelea kusaidia katika
maeneo mengine ya nchi ili kutatua suala la maji linaloikabili maeneo
mengi.
Mkurugenzi
wa halmashauri ya mji wa Handeni Thomas Mzinga alisema visima
vilivyofadhiliwa na mwenyekiti huyo, vitaweza kusaidia watu wapatao
5,000 ambao kutokana na kuwepo vioski hivyo vinavyozalisha maji lita
18,500 kwa siku na kuwafikia watu zaidi ya asilimia 40 ya wakazi wote wa
Chanika wapatao 9,000.
Mkurugenzi
huyo alisema kioski kilichokuwa sokoni ambacho kinahudumia masaa 24
kimekuwa kikiingiza kiasi cha sh. 20,700 kwa siku sawa na sh. 600,000
kwa mwezi hatua ambayo zinatosha kufanya ukarabati mdogo pindi uchakavu
unapotokea ili kuboresha huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment