Header Ads

Mchakato wa uandaaji wa sera ya Filamu wawavutia wasanii wa filamu nchini


Na: Genofeva Matemu - WHUSM

Wadau wa tasnia ya filamu nchini wameipongeza Serikali kuwashirikisha katika mchakato wa uandaaji na ukamilishaji wa Sera ya filamu nchini.

Hayo yamesemwa na wadau mbalimbali walioshiriki katika kikao cha kupitia uchambuzi wa hali halisi ya tasnia ya filamu kwa ajili ya maandalizi ya Sera ya filamu kilichofanyika mapema wiki hii.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo amesema kuwa sekta ya filamu hapa nchini imekuwa ikisimamiwa na kongozwa na Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 lakini kutokana na kukua kwa tasnia ya filamu ilionekena kuwa kuna uhitaji wa Sera ya Filamu itakayo kuwa dira na mwongozo katika kukuza tasnia hiyo.

Bibi. Fissoo amesema kuwa Bodi imekamilisha hatua ya uchambuzi wa hali halisi ya sekta ya filamu kwa kiasi kikubwa kwa kupitia machapisho mbalimbali pamoja na kuangaia mifano ya nchi zilizopiga hatua katika sekta ya filamu kama vile Afrika ya Kusini, Kenya, Nigeria pamoja na kuzingatia mchango mkubwa kutoka kwa wadau wenyewe ambao wamewezesha kupatikana kwa takwimu muhimu.

Aidha Muigizaji wa filamu nchini Bw. Saidi Jangala amesema kuwa sera inayoandaliwa iweke maelekezo ya kuzingatia utengenezaji wa filamu zinazobeba historia ya Kitanzania kama vile historia ya Majimaji, pia sera hiyo ianishe mikakati mahsusi ya upatikanaji wa mitaji pamoja na kuipa kipaumbele michezo ya kuigiza kwani michezo hiyo ndiyo chachu kuu ya weledi katika uigizaji.

Naye Msanii wa filamu nchini Bw. Chiki Mchoma ameiomba kamati ya kuanda sera ya filamu kuhakikisha sera inayoandaliwa inaelekeza wadau wa filamu kuandaliwa mifumo ya elimu pamoja na kuweka misingi ya kufilisi wanaojihusisha na uharamia wa kazi zao na kuwawajibisha wanaonunua kazi zitokanazo na uharamia.

Hata hivyo mtaalamu wa Kiswahili Pro. Hermas Mwansoko ameitaka kamati ya kuandaa sera ya filamu kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye filamu zetu kusaidia kuzitofautisha filamu za Kitanzania na zingine.

Kukamilika kwa sera ya filamu nchini kutabadilisha kabisha taswira nzima ya sekta ya filamu hapa nchini kwani itatoa dira ama mwelekeo wa tasnia. Hii itawezesha kuongezeka kwa fursa za uwekezaji katika tasnia, kuweka mwongozo kuhusu motisha na fursa za mitaji, uzalishaji wa bidhaa bora zenye kuzingatia weledi pamoja na filamu kuangaliwa kama chombo cha kukuza uchumi kwa manufaa kwa Taifa na watanzania wote.

No comments:

Powered by Blogger.