Waandishi wa habari wameaswa kuandika habari zenye tija kwa taifa.
Mkurugenzi wa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), Tawi la Dodoma Bw. Richard Wambali kifungua semina
iliyoandaliwa na benki hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari
katika kuandika na kutoa habari za sekta za uchumi, biashara na fedha maendeleo
yenye tija kwa taifa.
Meneja Msaidizi Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki Benki
Kuu ya Tanzania (BoT) Victoria Msina akimkaribisha Mkurugenzi wa BoT, Tawi la
Dodoma Bw. Richard Wambali wakati wa ufunguzi wa semina iliyoandaliwa na benki
hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuandika na kutoa habari
za za uchumi, biashara na fedha maendeleo yenye tija kwa taifa.
Baadhi ya washiriki wa semina wakimskiliza Mgeni rasmi Mkurugenzi
wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tawi la Dodoma Bw. Richard Wambali wakati wa ufunguzi
wa semina inayofanyika mjini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa
habari kuandika na kutoa habari za za uchumi, biashara na fedha maendeleo yenye
tija kwa taifa.
Mgeni rasmi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), Tawi la Dodoma Bw. Richard Wambali akiwa katika picha ya pamoja
na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa semina inayofanyika mjini Dodoma kwa
lengo la kuwajengea uwezo waandishi hao kuandika na kutoa habari za za uchumi,
biashara na fedha maendeleo yenye tija kwa taifa.
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Wanahabari nchini wameaswa kutumia taaluma yao vema katika kuhabarisha
umma kuhusu masuala ya uchumi, biashara na fedha kwa lugha ambayo wananchi wa
ngazi mbalimbali wataweza kuelewa kirahisi ili waweze kuchangia katika
maendeleo yenye tija kwa taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), Tawi la Dodoma Bw. Richard Wambali alipokuwa akifungua semina
iliyoandaliwa na benki hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari
katika kuandika na kutoa habari za sekta ya uchumi na fedha.
“Benki Kuu ya Tanzania inatambua na inathamini sana mchango
mkubwa unaofanywa na magazeti, vituo vya televisheni na radio kwa kutenga
nafasi maalum kwa ajili ya habari za fedha na uchumi na hasa zinatolewa na
Benki Kuu” alisema Bw. Richard.
Katika kuhakikisha vyombo vya habari vinatoa elimu katika
masuala ya fedha na uchumi, Bw. Richard amesema kuwa BoT imechukua jukumu la
kuwajengea uwezo wanahabari kila mwaka ili kuwaongezea uelewa wao kuhusu majukumu na kazi za Benki hiyo na mchango wake
katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Malengo mengine ya semina hiyo ni kuchochea na kukuza ari ya wanahabari katika
kuandika habari za uchumi na fedha, kutafsiri na kuchambua taarifa mbalimbali za uchumi na
fedha zinazotolewa na taasisi mbalimbali, kuwafahamisha wanahabari masuala yanayoendelea
katika uchumi wa Tanzania na wa dunia, mwelekeo wa uchumi na masuala ya fedha
katika siku zijazo na kuimarisha
uhusiano mzuri wa kikazi uliopo baina ya vyombo vya habari,
wanahabari na Benki Kuu.
Zaidi ya hayo, Bw.
Richard ameongeza kuwa Benki Kuu kama taasisi,
inajukumu la kujifunza namna vyombo vya habari vinavyofanya kazi na mahitaji yao katika kuandaa na
kuwasilisha taarifa na habari za uchumi na fedha.
Aidha, Bw. Richard amesema kuwa ukuaji wa uchumi nchini
unaoendelea sasa unatokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali na BoT
katika kutekeleza sera za uchumi na fedha pamoja na usimamizi wa uhakika wa
sera hizo.
“Kadiri uchumi unavyokua na kadiri mazingira ya biashara yanavyoendelea
kuvutia wawekezaji, mahitaji ya taarifa na habari sahihi na kwa wakati kuhusu
uchumi wa nchi yetu ikiwa ni pamoja na masoko ya fedha, uchumi wa kanda na
dunia kwa ujumla yanaongezeka sambamba na umuhimu wake” alisisitiza Bw. Richard.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa semina hiyo kwa niaba ya wanahabari
hao Ezekiel Kimwaga kutoka gazeti la Raia Mwema ameupongeza uongozi wa BoT kwa
kufikisha miaka 50 na kuishukuru benki hiyo kuthamini na kutoa fursa ya semina
hiyo kwa wanahabari kila mwaka ambayo inawaongezea uelewa katika masuala ya
uchumi na fedha.
Semina hiyo ya siku nne inajumuisha mada mbalimbali
zinazowasilishwa na wataalam kutoka BoT ni pamoja na kuzijua kurugenzi ambazo zinazohusika
na masuala ya uchumi, biashara na fedha ambazo ni Utafiti na Sera za Uchumi,
Masoko ya Fedha, Usimamizi wa Mabenki, Bodi ya Bima na Amana, Mifumo ya Malipo
ya Taifa na Huduma za Kibenki.
Mada nyingine katka semina hiyo ni kuzijua alama za usalama
zilizopo katika fedha, dawati la malalamiko ya wateja wa mabenki pamoja na
kuzijua kazi za matawi ya Benki Kuu ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment