Header Ads

UNDP YAZINDUA RIPOTI YA KAZI NA MAENDELEO YA BINADAMU, MAVUNDE AAGIZA KAZI YENYE STAHA

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) Antony Mavunde ametaka kuondolewa kwa changamoto maeneo ya kazi ili kazi isaidie maendeleo ya binadamu badala ya kujikimu.Naibu Waziri huyo alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuzindua ripoti ya maendeleo ya binadamu ya mwaka 2015 inayoelezea kazi kwa maendeleo ya binadamu.

Alisema kwa sasa kuna figisu kubwa katika kazi nchini hasa kutokana na waajiri wengi kugeuza kazi kama sehemu ya kujikimu kwa wafanyakazi wao kwa kutowapa stahiki husika ikiwamo mikataba ya ajira.

Alisema kazi inapokuwa ni ya kujikimu kunakuwa na migogoro mingi na kuvurugika kwa uzalishaji na kutishia maendeleo ya taasisi husika na maendeleo ya mtu binafsi.Alisema Tanzania imefurahishwa na yaliyomo katika ripoti hiyo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) kutokana na kuzungumzia jinsi kazi zinavyoweza kusaidia upatikanaji wa maendeleo.
UNDP HUMAN DEVELOPMENT REPORT 2015 LAUNCH
Mgeni rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Mh. Anthony Mavunde (katikati) akizindua rasmi Ripoti ya Maendeleo ya Watu ya mwaka 2015 (Human Development Report 2015) kwenye hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Machi 11, 2016.
Anthony Mavunde
Mgeni rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Mh. Anthony Mavunde akionyesha ripoti hiyo kwa wageni waalikwa na waandishi wa habari (hawapo pichani).
IMG_6200
Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Ofisi ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, Bi. Mary Kawar, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez, Mgeni rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Mh. Anthony Mavunde, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) nchini, Awa Dabo kwa pamoja wakiwa wameshikilia ripoti hiyo.
Alisema wakati Tanzania inaelekea kujipanga kwa uchumi wa kati, Ripoti inaonyesha ni jinsi gani kazi inaweza kuboresha maisha ya Mtanzanzania kwa kuondoa kazi na kuwapatia wananchi kazi zenye staha na zinazoweza kuwasaidia wao binafsi na hivyo kukuza uchumi na ustawi wa jamii.

Alisema amekuwa akizungumza katika maeneo mengi ya kazi na kukutana na changamoto nyingi zikiwemo za kukosekana kwa mikataba, mazingira mabaya ya kufanyakazi, ujira usiokidhi na kutaka waajiri kufuata sheria za kazi kwa kuwapatia mikataba ya kazi na pia kuhakikisha kazi zinakuwa na staha.

Awali akizungumza na wageni waalikwa katika hafla hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki mjini Dar es Salaam, alisema kwamba uzinduzi wa kitaifa ambao unafuatia uzinduzi wa kimataifa uliofanyika mwaka jana mjini Addis Ababa, Ethiopia ni faraja kubwa kwa wadau wa maendeleo nchini.Alisema uzinduzi huo unaweka ripoti hiyo karibu zaidi na wananchi na kuahidi serikali kuifanyia kazi kutokana na umuhimu wake hasa wa kuhakikisha kazi inasaidia maendeleo ya watu.

No comments:

Powered by Blogger.