Benki ya Exim yatangaza kupata ongezeko la faida ya asilimia 46
Afisa
Mkuu wa Fedha wa benki ya Exim Tanzania Bw. Selemani Ponda (katikati)
akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana
wakati akitoa taarifa ya mapato ya benki hiyo katika kipindi cha mwaka uliopita. Wengine ni NaibuAfisa Mkuu wa Fedha wa benki hiyo Bw. Issa Hamisi (kulia) na Mkaguzi Mkuu wa ndani wa hesabu za benki hiyo Bw. George Binde
BENKI
ya Exim Tanzania imetangaza kupata faida ya sh. bilioni 35.3 (kabla ya
kodi) kwa mwaka ulioipita 2015, sawa na ongezeko la faida kwa asilimia
46 ikilinganishwa na mwaka 2014 hatua iliyochagizwa na ufanisi wa benki hiyo katika usimamizi mizania.
“Kwa
kuangalia hali halisi ya changamoto mbalimbali katika masuala ya
kifedha ikiwemo masuala ya riba sambamba na kuporomoka kwa thamani ya
shilingi kwa muda wote, mafanikio haya tunayaona kuwa ya kuridhisha,’’
alisema Afisa Mkuu wa Fedha wa benki hiyo Bw Selemani Ponda alipokuwa
akitoa ripoti ya awali (kabla ya ukaguzi) ya benki hiyo mbele ya
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alisema katika kipindi hicho faida kwenye riba ilikuwa
kwa asilimia 28 na kufika sh. Bilioni 73 ikilinganishwa na kiasi cha
sh. 57 kilichopatikana katika kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita.
Ongezeko hilo limechagizwa na mkazo wa benki hiyo katika amana za
gharama nafuu, wingi wa matawi ya benki hiyo pamoja na usimamizi mzuri
wa mizania.
Zaidi,
tozo mbalimbali za huduma za kibenki katika kipindi cha mwaka ulioipita
kiliongezeka kwa asilimia 25 hadi kufikia sh bilioni 50, kutoka sh
bilioni 40 kilichopatikana mwaka uliopita.Ongezeko hilo pia lilichagizwa
na faida katika biashara ya kununua na kuuza fedha za kigeni pamoja na mapato mengine ya ada kutokana na ufanisi katika utoaji huduma kwa wateja wakubwa na wale wa kati.
Jumla
ya mapato yatokanayo na uendeshaji yaliongezeka kwa asilimia 29 hadi
kufikia sh. Bilioni 95 yakibebwa na ukuaji mkubwa kwenye ada pamoja na
kamisheni ambayo ilikuwa asilimia 29 kutoka sh bilioni 24 hadi sh.
Bilioni 31 kwa mujibu wa Bw Ponda huku akiongeza kuwa katika kipindi
hicho gharama za uendeshaji wa benki hiyo zilikuwa kwa asilimia 20 na
kufikia sh. Bilioni 80.
Benki
tanzu zilizopo nje nchini Djibouti na Comoro zimeendelea kufanya vizuri
na kuchangia asilimia 4 ya faida tofauti na mwaka jana zilileta hasara
kwa ujumla wao. Djibouti imefanya vizuri kulinganisha na mwaka uliopita
kwa kupata faida ya Sh bilioni 1.2. “Tunategemea benki hizi tanzu
kufanya vizuri zaidi mwaka 2016” aliongeza mkuu huyo wa fedha.
Bw
Ponda aliongeza kwamba katika kujiongezea mtaji wa biashara na
ushirikishaji wa wawekezaji wote nchini (financial inclusion), benki
hiyo hivi karibuni ilizindua uuzaji wa dhamana za muda mrefu (hati
fungani) ambapo hadi uuzwaji wa hati hizo unafungwa rasmi Disemba 18
mwaka 2015 benki hiyo ilikuwa imefanikiwa kukusanya kiasi cha sh bilioni
19.7 kutokana na mauzo ya hati hizo tofauti na makadirio ya sh. Bilioni
10 iliyokuwa imejipangia kukusanya hapo awali. Benki ya Exim imekuwa
taasisi ya kwanza kuzindua dhamana ya muda mrefu ikilenga wawekezaji
wadogo, wakati na wakubwa.
“Pia ni katika mwaka uliopita tumezindua
kituo chetu kipya cha huduma kwa wateja kwa njia ya mawasiliano ya
simu ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma zetu kupitia
teknolojia ya mawasiliano,’’
“Exim tunaahidi
kuendelea na muelekeo huu ulio sahihi kwetu na kwa wateja wetu katika
kutimiza malengo yetu. Ripoti hii inaonyesha kuwa mwaka uliopita ulikuwa
na mafanikio makubwa na ya kujivunia,’’ alisema Bw Ponda huku
akiwapongeza wafanyakazi na wadau wote waliochangia mafanikio hayo.
No comments:
Post a Comment