SERIKALI YASISITIZA MASHIRIKISHO YA MICHEZO KUZINGATIA UTARATIBU KUZUIA MIGOGORO.
SERIKALI
imetoa wito kwa Vyama,Vilabu na Mashirikisho ya mpira wa miguu
kuzingatia na kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa katiba zao ili
kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza katika uendeshaji na uendelezaji
wa soka nchini.
Hayo
yamesemwa Leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia Wambura (Pichani)wakati
akijibu swali la Mhe. Khatibu Saidi Haji Mbunge wa Konde (CUF) kuhusu
makosa yanayofanywa na klabu za soka nchini kwa kupeleka mambo ya
kisoka katika mahakama ambapo ni kinyume cha sheria za FIFA.
Mhe.
Annastazia Wambura amesema ni kweli kuwa Sheria za FIFA zinakataa mambo
yanayohusiana na soka kupekekwa mahakamani hivyo hatua hiyo ya Vyama na
Klabu kuzingatia Sheria na taratibu inalenga kuwezesha masuala ya soka
kuendeshwa kwa kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa na Mamlaka za
Michezo huo kwa ngazi mbalimbali.
Aidha
amesema hatua hiyo imewezesha mchezo wa soka kuchezwa na
kupata matokeo kwa wakati na hivyo kuepusha mazuio ya mahakama ambayo
yanaweza kusababisha usumbufu usio wa lazima kwa washiriki wengine hata
kupelekea kufungiwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF).
Maendeleo
ya michezo hapa nchini yanaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la
Michezo ya mwaka 1967, kama ilivyorekebishwa kwa mujibu wa Sheria Na 6
ya mwaka 1971 lakini bado Sheria hii inakinzana na Sheria za FIFA ila
serikali inafanya mapitio ya Sheria hiyo ili iendane na wakati kwa lengo
la kuboresha na kuendeleza michezo nchini.
SERIKALI KUANZISHA VYUO VYA VYA UVUVI KUONGEZA UJUZI KWA VIJANA
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
SERIKALI imekusudia
kuanzisha Vyuo vya Uvuvi katika maeneo yote yanayozungukwa na bahari
ili kuwafundisha vijana mbinu sahihi za kufanya shughuli za
Kilimo,Mifugo na Uvuvi ili kuwawezesha kukuza vipato vyao kwa kujiajiri.
Hayo
yamesemwa leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi Mhe.William Tate Ole Nasha akijibu swali la Mhe. Hamidu Hassan
Bolali Mbunge wa Mchinga (CUF) kuhusu umuhimu wa kujenga chuo cha uvuvi
mkoani Lindi ili kuwaongezea vijana ujuzi wa kazi hiyo.
Ameongeza
kuwa wizara inatambua umuhimu wa kuwafundisha vijana mbinu sahihi za
kufanya shughuli za uvuvi kilimo na ufugaji na kwa sasa wizara kupitia
Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvivu (Fisheries Education and Training
Agency (FETA) imeanzisha Chuo cha Uvuvi Mikindani Mtwara kwa lengo la
kusogeza huduma ya mafunzo ya uvuvi kwa wananchi hususani vijana walioko
ukanda wa kusini mwa Tanzania ukiwamo mkoa wa Lindi.
Mhe.William
Tate Ole Nasha amesema uanzishwaji wa Vyuo vya Uvuvi sio kwa maeneo
yanayozungukwa na bahari ila kwa maeneo mengine pia ili kuwezesha vijana
kupata ujuzi zaidi sio katika uvuvi pekee bali pia katika kilimo na
ufugaji, mbali na Chuo cha Uvuvi Mikindani Mtwara pia kuna vyuo vingine
kama vile Chuo cha Mbegani Mtwara chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 120
, Chuo cha Kibilizi Kigoma na Chuo cha Nyegezi Mwanza.
Mbali
za Vyuo hivyo serikali imehaidi kujenga vyuo Tanzania nzima ili
kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata kupata ujuzi zaidi katika Kilimo,
Uvuvi na Ufugaji ili kuendeleza ukuaji wa sekta hiyo na kuwezesha vijana
kujiajiri wenyewe kupitia mafunzo wanayapata.
Wakala
wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) itaanza kutoa mafunzo ya uvuvi
katika Chuo cha Uvuvi Mikindani ya muda mfupi kwa mwaka 2016/2017 na
yale ya Astashahada na Stashahada yataanza mwaka 20017/2018.
No comments:
Post a Comment