MBEYA INAWEZA KUPAA KIUCHUMI - WAZIRI MKUU

WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema mkoa wa Mbeya unaweza kupaa kiuchumi kama
utazingatia fursa za kibiashara ilizonazo na kuwekeza zaidi kwenye viwanda vya
usindikaji mazao ya kilimo na mifugo.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumatatu, Machi 2, 2015) wakati
akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Mbeya waliofika kusikiliza
majumuisho ya ziara yake ya siku saba kwenye mkoa huo. Mkutano huo ulifanyika
kwenye ukumbi wa Mkapa, jijini Mbeya.
“Nguvu
kubwa mnayo katika biashara hasa kama mtajitahidi kutumia vema fursa kubwa ya uwekezaji
katika viwanda vya kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo na mifugo mliyonayo,”
alisema.
Waziri
Mkuu alisema mkoa wa Mbeya katika msimu wa 2013/2014 umeweza kuzalisha tani
4,159,907 za nafaka na kuuwezesha kuwa na ziada ya chakula ya tani 3,347,680.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu alisema mkoa wa Mbeya bado una fursa nzuri ya kuongeza
uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na unaweza kuiwezesha kama nchi
kuuza chakula katika masoko ya Afrika na Afrika ya Mashariki kama watajipanga
vizuri.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu aliwapongeza viongozi hao
kwa kuuwezesha mkoa wa Mbeya kutoa mchango mkubwa katika Pato la Taifa. “Katika
taarifa ya mkoa, nimeelezwa kuwa mwaka 2013, mkoa huu ulichangia shilingi
trilioni 3.951 na hivyo kushika nafasi ya tatu kati ya mikoa yote nchini
ikitanguliwa na mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza.”
Alisema kutokana
na ukuaji wa kasi wa idadi ya watu ambao ni asilimia 2.7, mtu akichukua pato
hilo la mkoa na kuligawanya kwa idadi ya watu wa mkoa wa Mbeya anapata wastani
wa pato la kila mwananchi kuwa ni sh. 1,420,427. “Kipato hicho, ni sawa na shilingi
118,369 kwa mwezi au shilingi 3,946 kwa siku sawa na Dola za Kimarekani (US $)
2.3,” alifafanua.
Waziri Mkuu
alibainisha kwamba mtu akichukua wastani wa pato la kila mwananchi kwa mwaka
2013 na kupanga kwa mikoa yote, mkoa wa Mbeya unashuka na kushika nafasi ya
sita kitaifa. Aliitaja mikoa inayowatangulia kuwa ni Dar es Salaam sh.
1,990,043/- ambao ni wa kwa kwanza; wa pili ni Iringa (sh. 1,660,532/-); wa
tatu ni Arusha (sh. 1,448,782/-); wa nne ni Kilimanjaro (sh. 1,444,882/-); wa
tano ni Ruvuma (sh. 1,438,392/-) na wa sita ni Mbeya (sh. 1,420,427/-).
“Nawashauri
muongeze juhudi za kuipita mikoa hiyo kwa kuwa mna fursa nyingi za kuongeza
uzalishaji hasa katika mazao ya kilimo cha kahawa, kakao, mpunga, mahindi, viazi,
pamoja na mazao ya maliasili kama vile mazao ya misitu, na uvuvi na uchimbaji
madini,”.
Waziri
Mkuu amemaliza ziara yake ya siku saba mkoani Mbeya leo kwa kufanya majumuisho ya
ziara yake na amerejea jijini Dar es Salaam jana jioni (Jumatatu, Machi 2, 2015) .
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MACHI 3, 2015.
No comments:
Post a Comment