BARAZA la Habari Tanzania (MCT) limekubali kuanza ushirikiano na uhusiano mzuri na Chama cha Bloggers Tanzania (TBN)
Kauli
hiyo imetolewa juzi jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa MCT,
Kajubi Mkajanga alipokuwa akizindiwa hafla ya kwanza ya mwaka 2015 ya
wamiliki na waendeshaji wa blogu na mitandao mingine ya kijamii
iliyofanyika katika Hoteli ya Serena.
Katibu
huyo Mtendaji wa MCT alisema kwa maendeleo ya sasa ya teknolijia ya
habari na mawasiliano ni vigumu kuzitenga blogu kama vyombo vya habari,
hivyo kuahidi kushirikiana na TBN kuhakikisha inafikia malengo yake ya
kuwaunganisha bloggers na kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili.
Alisema
MCT inasubiri TBN ipate usajili kisheria toka mamlaka husika serikalini
na baada ya zoezi hilo itaanza kushirikiana maramoja na chombo hicho
kilichoanzishwa kuwaunganisha wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya
kijamii nchini na wale wanaofanya shughuli za nje ya nchi.
"...MCT
ipo tayari wakati wowote kuanza kushirikiana nanyi kikazi,
tunachosubiri ni TBN kusajiliwa rasmi...mtakapo maliza usajili tu njooni
ofisi, tutazungumza na viongozi wenu ili kujua nini cha kuwasaidia.
Naombeni msichelewe tuanze hili mara moja," alisema Kajubi Mkajanga
akizungumza na wana-TBN kabla ya kuzinduwa sherehe hiyo.
Awali
akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa TBN, Joachim Mushi alisema
kwa sasa mitandao ya kijamii imekuwa ikitekemewa na kundi kubwa la jamii
katika kusambaza taarifa kwa haraka licha ya uwepo wa changamoto kadhaa
ndani ya tasnia hiyo.
Alisema
pamoja na mambo mengine, TBN imeanzishwa kwa lengo la kuwaunganisha
waendeshaji na wamiliki wa blogu pamoja na mitandao mingine ya kijamii,
na pia kuhakikisha wana-TBN wanapata fursa ya kujifunza zaidi maadili ya
tasnia ya habari na mawasiliano ili kufanya kazi zao kiufanisi zaidi.
No comments:
Post a Comment