SERIKALI YAJIDHATITI UHIFADHI NA KULINDA KUMBUKUMBU ZA URITHI WA TAIFA
Mkurugenzi
wa Mambo ya Kale toka Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Donatius
Kamamba(kushoto) akieleza kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu
mikakati ya serikali katika kulinda na kuhifadhi kumbukumbu na urithi
wa Taifa, wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya
Habari(MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.Kulia ni Afisa Habari wa Idara
ya Habari (MAELEZO) Bi.Fatma Salum.Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano toka Wizara ya Maliasili na Utalii Bi.
Doreen Makaya(kushoto) akiongea na waandishi wa habari(hawapo pichani)
akiwataka kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuzuia ujangili.Kulia ni
Mkurugenzi wa Mambo ya Kale toka Wizara Hiyo Bw. Donatius Kamamba.
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
IDARA YA MAMBO YA KALE
KUMBUKUMBU NA URITHI WA TAIFA
Wizara,
kupitia Idara ya Mambo ya Kale, inao wajibu wa kutambua, kulinda,
kutunza na kuhifadhi Kumbukumbu na Urithi wa Taifa na Urithi wa Dunia
kwa mujibu wa Sera ya Malikale ya 2008, Sheria ya Mambo ya Kale Sura 333
(R.E 2002) na Mkataba wa Kimataifa wa 1972 wa UNESCO. Kumbukumbu na
Urithi huu unatokana na rasilimali za Utamaduni zinazoshikika na
zisizoshika; zinazohamishika na zisizohamishika kama zinavyoainishwa
katika Sera ya malikale (2008), Sheria ya Mambo ya Kale, Sura 333.
Wizara,
kwa maana ya Idara ya Mambo ya Kale, ili kutekeleza azma hii inao
wajibu, kwa kuwashirikisha wamiliki wa Urithi huu, kufanya na kuratibu
Utafiti; kutambua umuhimu wa malikale husika kihistoria, kiimani,
kisayansi, kisiasa na kiuchumi. Wizara, kupitia Idara ya Mambo ya Kale
inalo jukumu la kutambua, kulinda, kutunza, kuhifadhi Kumbukumbu na
Urithi wa Taifa na ule wa Dunia kwa mujibu wa Katiba ya nchi (1977);
Sera ya Utamaduni 1999; Sera ya Malikale (2008) na Sheria ya Mambo ya
Kale, (Sura 333). Aidha, Serikali ya Tanzania imeridhia mikataba ya
Kimataifa ya UNESCO ya mwaka 1954, 1970 na 1972.
Malengo
mahususi ya Sera ya Malikale 2008 ni pamoja na kufafanua dhima na
majukumu ya Serikali za mitaa, jamii, watu binafsi, mashirika na asasi
mbalimbali katika kuhifadhi na kusimamia malikale; kuweka ufafanuzi
sahihi wa kulinda, kusimamia, kutunza, kuhifadhi, kuendesha na
kuendeleza malikale; kuweka Kumbukumbu za Urithi wa Taifa kwa ujumla,
na kuainisha namna bora ya kusimamia utafiti na uhifadhi wa malikale.
Sera
imeweka bayana kuwa suala la urekebu kuhusu utafiti na uhifadhi wa
Urithi wa Taifa utafanywa na Serikali. Aidha, suala la uhifadhi na
uendelezaji malikale linahusisha sekta mbalimbali katika jamii na jamii
kwa ujumla. Wizara kwa kuwashirikisha wadau inakamilisha utaratibu wa
kutunga sheria mpya kuhusu malikale ili Sera iweze kutekelezeka.
Kimsingi,
Urithi tegemewa (Potential heritage) wa Utamaduni unatengenezwa kila
siku kutokana na kazi za binadamu wakati wa kupambana na mazingira ili
kukidhi mahitaji yake. Aidha, kwa msingi huo huo, Urithi tegemewa
hutoweka kila siku. Kwa mujibu wa misingi ya uhifadhi, umri wa miaka
100 na zaidi huonekana kuwa ni kigezo na ni msingi muhimu. Hata hivyo,
umri pekee yake hautoshi ni lazima umuhimu wake nao uainishwe na
uwekwe bayana.
Wizara
hutenda yote hayo kwa ajenda ya kuhakikisha kuwa vielelezo halisi vya
chimbuko na maendeleo ya binadamu vinarithishwa kutoka kizazi kimoja
kwenda kijazi kingine.
No comments:
Post a Comment