BABU WA LOLIONDO AINENEA MAZITO TANZANIA, AMWELEZA MIZENGO PINDA MAMBO ALIYOOTESHWA NA MUNGU
MCHUNGAJI Ambilikile Mwaisapila wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) amesema Mungu ameendelea kujifunua kwake na
kumuonyesha kuwa Tanzania itakuwa kioo cha Afrika na baadaye kioo cha
dunia.
Ametoa kauli hiyo jana asubuhi (Jumanne, Septemba 24, 2013)
mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akizungumza na wakazi wa
kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakati msafara wa
Waziri Mkuu uliposimama nyumbani kwake ili kumsalimia akiwa njiani
kurejea mjini Arusha.
Mchungaji Mstaafu Mwaisapila maarufu kama Babu wa Samunge
alisema kuna mambo mengi ambayo yameandikwa kwenye Biblia lakini
hayakutokea Israeli na sasa yatafanyika hapa Samunge. “Mungu ametupenda
sana, yanakuja mambo makubwa na wala hayako mbali. Kama mimi ni mzee na
nitayaona, kwa hiyo mtarajie kuwa hayako mbali kutokea,” alisema huku
akishangiliwa.
Alisema katika mafunuo aliyopewa na Mungu ameonyeshwa kwamba
watu wengi zaidi watafurika kijijini Samunge kuliko ilivyokuwa hapo
awali. Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa misaada iliyotoa
wakati wa ‘kugawa kikombe’ ikiwemo mahema, maji na ulinzi.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara maalum ya
kusikiliza matatizo ya ardhi yanayowakabili wakazi wa wilaya ya
Ngorongoro, katika tarafa za Ngorongoro, Loliondo na Sale alisema
anakubaliana na utabiri wa Mch. Mwaisapila kwani Tanzania imejaliwa gesi
nyingi na mafuta mengi ambavyo vitabadili sura ya Taifa hili.
“Mungu ametupa gesi nyingi sana, katika miaka miwili
tutakuwa na umeme kila mahali. Tuna makaa ya mawe ambayo ni nishati
kubwa na sasa tuna fursa ya kupata nishati ya umeme kutoka ardhini
(geo-thermal) katika Ziwa Natron,” alisema.
Alisema Tanzania imekuwa kimbilio la kila mwekezaji na sababu kubwa ni amani na utulivu uliopo nchini.
Aliwaeleza wakazi wa Samunge kwamba mapema mwakani
mkandarasi wa barabara atakuwa katika eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa
barabara ya lami ambapo awamu ya kwanza itaanzia Wasso hadi Mto wa Mbu
kupitia Samunge.
Akitoa ombi maalum kwa niaba ya vijana mbele ya Waziri Mkuu,
Bw. Elias Kalumbwa alisema wanaomba kuchimbiwa bwawa ili waweze
kujiajiri kupitia kilimo cha mbogamboga na matunda.
Bw. Kalumbwa ambaye amesomea masuala ya wanyamapori alisema
eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto wa msimu unaopita kijijini hapo.
“Eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto wetu, vijana tunaweza kujiajiri
endapo tutapata bwawa ili tufanye kilimo cha umwagiliaji maji,” alisema
huku akishangiliwa.
Naye Bibi Martha Sereri (70) alimweleza Waziri Mkuu kwamba
wanaomba jimbo la Ngorongoro ligawanywe kwa sababu ni kubwa sana kiasi
kwamba inamuwia vigumu mbunge wao kufika maeneo yote. Aliomba pia
wapatiwe walimu wa sayansi na hisabati kwa ajili ya shule 10 za
sekondari zilizopo kwenye tarafa yao.
Aliomba wapatiwe mikopo ya matreka ili waweze kuongeza
ukubwa wa mashamba yao. “Tunaomba mikopo ya matrekta na plau, haya
mashamba umeyaona njiani yamelimwa na Wakenya. Ukikodisha trekta kila
ekari unatozwa sh. 100,000/-. Je tutafika wapi? Mkitukopesha matrekta
mtakuwa mmetusaidia zaidi,” alisema.
Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu alisema hoja zao ni za msingi
na kwamba suala la vijana kupatiwa bwawa ni jambo linalowezekana
kupitia mipangpo ya maendeleo ya kilimo ya wilaya (DADPS).
“Andaeni andiko lenu, inabidi litoke kwa wananchi na siyo
Serikalini. Mkituletea ni jambo linalowezekana kwani liko ndani ya
mipango ya wilaya.”
Akijibu hoja kuhusu ukubwa wa jimbo, Waziri Mkuu aliwaambia
wakazi hao kwamba inawezekana kuongeza jimbo isiwe suluhisho la matatizo
yao kwa sababu ya jiografia ya eneo lao.
“Kuongeza jimbo inaweza isiwe jibu la kila kitu kwani
matatizo mnayopata yanatokana na jiografia ya eneo lenu, kutoka
Ngorongoro, Loliondo hadi huku Sale. Mimi nadhani tuangalie pia
uwezekano wa kuwapa Halmashauri ili kusogeza huduma kwa wananchi.
Tutaangalia njia zote mbili na kuona ipi italeta majibu ya haraka
kwenu,” alisema.
No comments:
Post a Comment