BAKITA yampongeza Rais Dkt. Magufuli kwa matumizi ya Lugha ya Kiswahili.
Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Baraza la Kiswahili la Taifa(BAKITA), Prof.Martha Qorro(Kulia)
akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari ambapo wamempongeza Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa uzalendo
wake wa kuitumia lugha ya Kiswahili katika mikutano mikubwa ya kitaifa ikiwemo
mkutano wa 17 wa nchi wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki , katikati ni
Katibu Mtendaji wa BAKITA Dkt. Seleman Sewangi na kushoto ni Afisa Habari wa
Idara ya Habari(MAELEZO) Bi.Lorietha Laurence.
Katibu Mtendaji wa
Baraza la Kiswahili la Taifa(BAKITA),Dkt. Seleman Sewangi akionyesha kamusi
Kuu ya Kiswahili kwa waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa uzalendo wake wa kuitumia lugha
ya Kiswahili katika mikutano mikubwa ya kitaifa ukiwemo mkutano wa 17 wa nchi
wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza
la Kiswahili la Taifa(BAKITA), Prof.Martha Qorro na kulia ni wake
Mkurugenzi,Taasisi ya Taaluma za Kiswahili chuo kikuu cha Dar es Salaam Dkt.
Ernesta Mosha .(Picha na Eliphace Marwa-maelezo).
Na
Lorietha Laurence-Maelezo.
Baraza
la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli kwa uzalendo wake wa kuitumia lugha ya
Kiswahili katika mikutano mikubwa na hafla mbalimbali za kitaifa na kimataifa.
Akiongea
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
BAKITA, Prof. Martha Qorro ameeleza msimamo huo wa Rais Dkt.Magufuli umewasidia Watanzania kupata taarifa moja kwa
moja kutoka tukio husika.
“Uamuzi
na msimamo wa Rais Magufuli wa kutumia lugha ya Kiswahili katika mikutano
mikubwa ikiwemo mkutano mkuu wa 17 wa
viongozi wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepokelewa
kwa furaha kubwa na wananchi na wadau wengi wa Kiswahili ndani na nje ya
Tanzania” alisema Prof.Martha.
Aliongeza
kuwa kupitia msimamo huo wa Mhe. Rais Magufuli, Baraza linaamini kwamba hatua hiyo itasaidia
kukuza lugha ya Kiswahili na kutoa fursa ya ajira kwa Watanzania kupitia
tafsiri na ukalimani na hivyo kuwapelekea maendeleo wananchi wote wa Afrika
Mashariki.
Naye
Katibu Mtendaji wa BAKITA Dkt. Seleman Sewangi ametoa wito kwa viongozi wengine
wa ngazi mbalimbali za Kitaifa kufuata nyao za Mhe.Rais Magufuli kwa kuipa
kipaumbele lugha ya Kiswahili ili kufikisha ujumbe kwa Watanzania walio wengi.
“Natoa
wito kwa viongozi wetu wa ngazi mbalimbali za kitaifa kuitumia lugha ya
Kiswahili katika mikutano mikubwa na hafla mbalimbali za kitaifa na kuachana na
dhana ya kutumia lugha ya kigeni yenye lengo la kuwafurahisha wageni wachache”
alisema Dkt. Sewangi.
Aidha,
aliongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa lugha ya kiswahili inatumiwa vizuri,
Baraza hilo linaendelea kutekeleza mkakati wa kukamilisha kanuni
zitakazopelekwa bungeni ili kumuwezesha Waziri mwenye dhamana kuwa na mamlaka
ya kusimamia sheria ya lugha ya Kiswahili ya mwaka 1961 iliyorekebishwa mwaka
1985 ili kuipa nguvu ya kumshitaki mtu yeyote kwa matumizi mabaya ya lugha hiyo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi,Taasisi ya Taaluma za Kiswahili chuo kikuu cha Dar es
Salaam Dkt. Ernesta Mosha ameziomba ofisi za Serikali hususani mahakama kutumia
lugha ya Kiswahili kwa kuwa ni lugha inayoeleweka na Watanzania wengi ikizingatiwa
kuwa sio wote wanajua kutumia lugha ya kiingereza.
No comments:
Post a Comment