WAZIRI MKUU MAJALIWA AHUDHURIA IBADA YA KUMUINGIZA KAZINI MKUU WA KKKT TANZANIA ASKOFU SHOO MJINI MOSHI.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea picha aliyopewa na Askofu Mkuu Mpya wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheli,Askofu Frederck Shoo katika ibada ya
kumuingiza kazini askofu huyo ilyofanyika kwenye kanisa kuu la KKKT
mjini Moshi Januari 31, 2016.
Baadhi
ya waalikwa walioshiriki katika ibada ya kumuingiza kazini Mkuu wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo
iliyofanyika kwenye kanisa kuu la KKKT mjini Moshi Januari 31, 2016.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizunguza katika ibada ya kumuingiza kazini Mkuu
wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick
Shoo iliyofanyika kwenye kanisa Kuu la KKKT mjini Moshi Januari 31,
2016.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa
katika ibada ya kumuingiza kazini Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania, Askofu Frederick Shoo kwenye kanisa Kuu la KKKT
mjini Moshi Januari 31, 2016.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo (kulia) na Askofu
Mkuu wa KKKT Mstaafu Alex Malasusa baada ya ibada ya kumuingiza kazini
Askofu Shoo iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la KKKT mjini Moshi Januari
31, 2016.
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema suala la ada elekezi linaendelea kufanyiwa
kazi na Serikali na likifika hatua nzuri litahusisha wadau wote ili
kupata maoni yao.
Ametoa
ahadi hiyo leo mchana (Jumapili, Januari 31, 2016) wakati akizungumza
na mamia ya waumini walioshiriki ibada ya kumuingiza kazini Mkuu Mpya wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick
Onaeli Shoo iliyofanyika kwenye usharika wa Moshi Mjini, Dayosisi ya
Kaskazini.
Waziri
Mkuu Majaliwa ambaye alihudhuria ibada hiyo kwa niaba ya Rais Dk. John
Pombe Magufuli alikuwa akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Dk. Shoo
ambaye alisema kama Serikali inataka kuondoa ada elekezi haina budi
kuziimarisha shule zake ili ziwe kama zilivyokuwa zamani.
Akijibu
hoja kuhusu miundombinu ya reli, Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua
kufufua miundombinu hiyo na kwamba hivi sasa inafanya mapitio ili kujua
gharama halisi kwa maeneo husika. Alisema Serikali imepanga kuanza na
maeneo manne ambapo la kwanza alilitaja kuwa ni reli ya kutoka Dar es
Salaam – Mwanza – Tabora – Kaliua – Mpanda hadi Karema.
“Eneo
la pili ni reli ya ukanda wa Kaskazini ambayo itatoka Dar es Salaam –
Tanga – Arusha hadi Musoma. Ya tatu ni ya kutoka Tabora – Kahama –
Kigali (Rwanda) na kuishia nchini Burundi ambayo tunataka isaidie
kusafirisha mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam. Reli ya nne ni ile
ya kutoka Mtwara kupitia Tunduru kwenda Songea hadi Mbamba Bay,”
alisema.
Kuhusu
ulinzi wa demokrasia ndani ya Bunge, Waziri Mkuu alisema anakubaliana
na Askofu Dk. Shoo juu ya mihimili yote mitatu kuheshimiana na kwamba
ameshukuru kwamba ameonya juu ya lugha zinazotumika ndani ya Bunge.
“Bunge
ni eneo linaloweza kujenga jamii mpya kwa sababu Bunge ni kioo na jamii
ya Watanzania inatuangalia sisi tuliomo mle. Ni vema tuwe na lugha
nzuri, tabia njema na hata jinsi tunavyovaa ili wanaotuona wapate hamu
ya kuiga,” alisema.
Kuhusu
ombi la kuibuliwa upya mchakato wa Katiba mpya, Waziri Mkuu alisema
suala hilo amelichukua na anaenda kulifanyia kazi. “Nakuhakikishia Baba
Askofu ushauri ulioutoa kwa Serikali tumeupokea,” alisisitiza.
Mapema,
akitoa hotuba yake, Askofu Mkuu Dk. Shoo alisema Bunge ni nyumba ya
demokrasia kwa hiyo jamii inatarajia kuona hoja zikijadiliwa kwa haki na
amani badala kutumia ubabe na mabavu au nguvu ya dola.
“Nimewaona
baadhi ya wabunge mko hapa… hili ninalolisema ni lenu na linawahusu
ninyi na spika wenu. Wabunge tunzeni heshima yenu na Mungu awasaidie
kulitimiza hilo. Wewe Waziri Mkuu ni Msimamizi wa shughuli za Serikali
bungeni kwa hiyo una kazi ya kusimamia. Kila mhimili unapaswa utunze
heshima yake…,” alisisitiza.
Kuhusu
Katiba mpya, Askofu Dk. Shoo alisema Watanzania wengi wana kiu ya kuona
mchakato huo ukiibuliwa upya na kukamilishwa ili nchi ipate Katiba mpya
yenye kukidhi kiu ya watu wake na inayoheshimu matakwa ya wengi.
“Mchakato
huo ukianza utumike kuganga majeraha yote yaliyopita. Tukifanya hivyo
tutakuwa tumeisaidia Serikali ya Awamu ya Tano kuipelekea nchi yetu kule
ambako imedhamiria. Yote yanawezekana tukitaka na tukipenda,”
alisisitiza.
Kwa
upande wake, Askofu ambaye amemaliza muda wake wa kuliongoza kanisa
hilo, Dk. Alex Malasusa alisema anamshukuru Mungu kwa kupata kibali cha
kushuhudia Mkuu mpya wa kanisa hilo akipokea kijiti cha uongozi kutoka
kwake.
“Si
kwa akili na uwezo wangu bali ni kwa uweza wa Mungu kwamba nimeweza
kuishuhudia siku ya leo. Ninamuomba Mungu akusaidie kuongoza kanisa
hili, akusaidie kukemea na kuonya kwa upole. Najua Mungu atakupunguzia
hata marafiki kwa sababu ya matamshi utakayokuwa ukiyatoa, lakini si
wewe bali ni uweza wa Bwana na roho mtakatifu anayekuongoza,” alisema.
Aliahidi
kuendelea kuwaombea Rais Magufuli pamoja na Waziri Mkuu Majaliwa katika
majukumu waliyonayo. “Msiogope kwa ajili ya majukumu mliyopewa, msihofu
tunaendelea kuwaombea kwa sababu tuko pamoja na sisi ni sehemu ya
utumishi wa Taifa,” alisema.
Waziri Mkuu anarejea Dodoma jioni hii kuendelea na vikao vya Bunge.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JANUARI 31, 2016.
(PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
No comments:
Post a Comment