Header Ads

Soma Hotuba ya kufunga mwaka ya Mhe: Zitto Kabwe (Mb), wakati wa mkutano wa pamoja wa hadhara na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, mjini Mtwara

 Mbunge wa Kigoma Kaskazini-Chadema Zitto Kabwe
---
Hotuba ya kufunga mwaka ya Mhe: Zitto Kabwe (Mb), wakati wa mkutano wa pamoja wa hadhara na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, mjini Mtwara (31/12/2014).

Ndugu Profesa Ibrahimu Lipumba

Mwenyekiti wa Taifa wa CUF,

Ndugu Viongozi mbalimbali mliopo hapa leo,

Ndugu Wananchi

Mtwara Hakiii

Mtwara kuchele? Mtwara kumekucha?


MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, nashukuru sana kwa mwaliko wako kuja kuzungumza na watu wa Mtwara na kujumuika nao katika kufurahia mafanikio makubwa waliyoyapata katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Nakushukuru kwa kipekee kwa upendo wako kwangu. Umekuwa mlezi wangu kisiasa na kimaisha. Hata pale nilipopitia mikiki mikiki na mihemko ya kisiasa, kamwe hukunikatia hukumu, bali uliona namna bora zaidi ya kunijenga kiuongozi. Wakati baadhi ya watu wakiandikia tanzia yangu ya kisiasa, uliniita na kufuturu nawe nyumbani kwako ukiwa katika moja ya sunna zako unazofunga kila wiki. Nakushukuru sana sana, na ninaomba uendelee kunilea katika maisha yangu ya kisiasa, kifamilia, kijamii na hata kitaaluma. Ukiwa mbobezi wa kimataifa katika taaluma ya uchumi nami nafuata nyayo zako, nataka nipite humohumo ulimopita na inshallah na hata zaidi.

Ndugu wananchi,

Ni kwa sababu ya upendo wa Profesa Lipumba kwangu nilishindwa kukataa kukubali mwaliko wake kuja hapa kujumuika nanyi katika siku hii muhimu sana. Hakuna namna bora zaidi ya kushukuru zaidi ya kuendelea kufanya kazi pamoja katika kuwatetea Watanzania na Tanzania yetu. Umoja wa upinzani ndio silaha dhidi ya mabwenyenye wa kiuchumi na kisiasa hapa nchini. Najua huko waliko inawauma sana wanapoona wapinzani wanaungana bila kujali tofauti ndogondogo zinazojitokeza miongoni mwao. Tutaendelea kushirikiana kwa maslahi mapana ya nchi yetu na katika kuhakikisha kwamba utawala wa Chama cha Mapinduzi ambacho sasa ni chama cha mabwenyenye unakoma katika nchi yetu mapema iwezekanavyo.

Nimekuja pia Mtwara kwa sababu huu ni Mkoa wa kipekee katika historia ya nchi yetu. Mtwara ni Mkoa ambao kwa miaka zaidi ya miaka 25 baada ya nchi yetu kupata uhuru ulibaki kuwa ngome imara dhidi ya mabeberu wa Kireno na waasi wa nchi jirani ya Msumbiji. Wakati mikoa mingine ikisonga mbele katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Mikoa ya Mtwara na Lindi ilibaki nyuma kwa sababu ya kulinda heshima ya mipaka ya nchi yetu. Hii ni historia muhimu sana ambayo vijana wetu inabidi waijue na waithamini.

Katika miaka ya hivi karibuni Mkoa wa Mtwara umechukua sura mpya kabisa kitaifa kufuatia kugunduliwa kwa gesi. Na katika hili wananchi wa Mtwara mmeonyesha kwamba watanzania wanaweza kupigania maslahi ya Taifa wakiamua. Mmesimama kidete kuhakikisha kwamba utajiri huu hauporwi na kwamba haturudii makosa yaliyofanyika Kanda ya Ziwa pale tuliporuhusu madini kuporwa na mabeberu wa kimagharibi kwa msaada wa mabwenyenye uchwara nchini mwetu. Nyie wananchi wa Mtwara mmesimama kidete katika kulinda maliasiali hii iliyogunduliwa kwa niaba ya wananchi wenzenu nchi nzima ya Tanzania.

Najua bado mnalia kuhusu Bomba la kupeleka Gesi Asili Dar es Salaam. Machozi yenu yatafutika tu kwani tayari habari za ufisadi mkubwa katika ujenzi wa Bomba hili zimeanza kuchomoza. Kiongozi wa Upinzani Bungeni ametamka mara kadhaa kuwa atatoa hoja kuhusu ufisadi katika ujenzi wa Bomba la Gesi. Sisi wengine, pale atakapohitaji msaada wetu, tutamsaidia kwani tunaamini gharama za mradi huu zimezidishwa mara mbili na inawezakana kabisa kuwa zaidi ya dola za Marekani 600 milioni zimegawanywa kwa watu kama rushwa kuanzia Uchina mpaka hapa Tanzania. Machozi yenu wana Mtwara yatafutwa tu, kwa uwezo wa mola.

Kwa hiyo kwangu mimi Mtwara ni alama ya harakati za kupigania haki za wananchi kumiliki, kuendesha na kufaidika na mali asili za Taifa. Tutaendelea kushirikiana nanyi kuhakikisha kwamba utajiri unaoendelea kugunduliwa hapa Mtwara na Tanzania kwa ujumla unasaidia wananchi katika kuboresha maisha yao, elimu zao na kumaliza umaskini.

Mimi kama mwana michezo na ambaye napigania maendeleo na mafanikio ya timu za hapa nyumbani Tanzania, niwapongeze pia wana Mtwara kwa sababu ya timu yenu ya mpira ya Ndanda FC ambayo imeleta changamoto sana kwenye maendeleo ya soka nchini kwetu. Napenda kuitakia kheri timu yenu ya Ndanda FC katika mashindano ya Ligi Kuu ya Tanzania yanaendelea hivi sasa.

No comments:

Powered by Blogger.