Header Ads

ASEMA HAJAONA RIPOTI ALIYOWAPA WAANDISHI, AELEZA RIPOTI YA UGONJWA ANAYO DK MWAKYEMBE MWENYEWE, DK SLAA NAYE ASEMA ,"SINA IMANI NA MANUMBA"
Waandishi Wetu
WINGU zito limetanda kuhusu afya ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe baada ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda, kusema kuwa ripoti ya ugonjwa wa Mwakyembe, anayo mwenyewe na kwamba wizara haina ripoti iliyotolewa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba, kwa waandishi wa habari.

Lakini wakati Dk Mponda akitoa kauli hiyo, baadhi ya watu wa kada tofauti wakiwamo viongozi wa dini na wasomi, wamekosoa ripoti hiyo ya polisi.

Mmoja wa watu hao, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa alisema,"hata mimi simwamini Manumba."

Malumbano hayo yanakuja wakati Dk Mwakyembe ambaye ni pia ni Mbunge wa Kyela, akitarajiwa nchini jana kwenda India kwa matibabu katika Hospitali ya Apollo.

Mahojiano na Waziri Mponda

Gazeti: Salaam Mheshimiwa waziri. Nimekupigia kutaka ufafanuzi kuhusu ripoti iliyotolewa na DCI Manumba kuhusu ugonjwa wa Dk Mwakyembe. Ninyi wizara mnaitambuaje?

Waziri: Kiutaratibu ripoti ya daktari ni ya mgonjwa. Sisi hatujaandika ripoti, muulizeni DCI Manumba awape ufafanuzi kama kuna kitu mnataka kuuliza zaidi kwa alichokizungumza na ninyi waandishi.

Gazeti: DCI Manumba alitoa taarifa kwa waandishi lakini aki-refer (rejea) ripoti kutoka wizarani (afya), baada ya kuwasiliana nanyi, kwa nini wewe usiizungumzie?

Waziri: Narudia tena, muulizeni yeye DCI au Dk Mwakyembe mwenyewe, wao wanaweza kuwapa ufafanuzi.

Gazeti: Tayari Dk Mwakyembe mwenyewe amekwishatoa tamko kwamba ripoti iliyosomwa na polisi, haina uhusiano na ripoti aliyokuwa nayo yeye kuhusu uchunguzi wa maradhi yake. Je, ripoti hii ya polisi ambayo wamedai wameipata kwenu (wizara) mmeitoa wapi?

Waziri: Ni hivi, baada ya daktari kumchunguza mgonjwa, hutoa ripoti na kumpa mgonjwa. Kwa hiyo, ripoti ya Hospitali ya Apollo anayo Dk Mwakyembe mwenyewe. Tena yeye kaeleza vizuri kabisa kwamba hata uchunguzi bado unaendelea. sasa hapo mnataka niseme nini tena?

Gazeti: Sasa kama ripoti anayo Dk Mwakyembe mwenyewe na tayari amesema ripoti ya polisi waliyosema imetoka kwenu siyo sahihi, je wizara iliwahi kupata ripoti ya Hospitali ya Apollo.

Waziri: Sisi tulichokifanya ni kumpa rufaa Dk Mwakyembe kwenda India. Ripoti hadi sasa anayo mwenyewe ingawa huwa tunapata taarifa baada ya yeye mgonjwa kuzileta kwetu. Hizo ndizo kanuni za taaluma ya udaktari, kwa hiyo ripoti anayo mwenyewe.

Gazeti: Sasa kama ripoti anayo Dk Mwakyembe mwenyewe, hii iliyosomwa na DCI imetoka wapi?

Waziri: Kumbuka DCI ana njia zake nyingi za kupata taarifa. Kwa hiyo ndiyo maana nasisitiza, muulizeni mwenyewe awape ufafanuzi kwa aliyozungumza na waandishi. Sisi wizara mnatuonea tu.

Gazeti: Lakini, hata kama ugonjwa ni siri, huoni mheshimiwa waziri kwamba kuna haja ya kuondoa utata kuhusu suala hili ikizingatiwa kuwa Dk Mwakyembe ni kiongozi anayegusa hisia za watu tofauti?

Waziri: Wanaoweza kuzungumzia maradhi yake, ni familia yake au yeye mwenyewe kwani ndiye mwenye ripoti. Mtafuteni au iulizeni familia yake iwapatie majibu. Lakini wizara haiwezi kufanya hivyo. Narudia tena, kuhusu hilo la DCI muulizeni mwenyewe awape ufafanuzi, mimi sijaona ripoti ya DCI aliyozungumza na waandishi wa habari.

Alichosema DCI

Akizungumza na waandishi mwishoni wa wiki iliyopita, Manumba alisema, “ukweli kuhusu kauli hiyo inayodai kuwekewa sumu, tumeupata baada ya kuwasiliana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambayo nayo imewasiliana na hospitali aliyokuwa amelazwa Dk Mwakyembe nchini India. Taarifa zinaonyesha kuwa hakuna sumu."

Jana, alipoelezwa kwamba Dk Mwakyembe ameikana ripoti yao, Manumba alisema "sasa suala hilo litashughukiliwa kisheria."

Alisisitiza kuwa suala hilo litashughulikiwa kwa kufuata misingi ya kisheria na kwamba, Jeshi la Polisi haliko tayari kuendeleza malumbano kupitia vyombo vya habari.

"Hatua zaidi zinachukuliwa dhidi ya jambo hilo, kwa sasa litashughukiliwa kwa kufuata misingi ya kisheria kama nilivyokwishaeleza awali,"alisema Manumba.


Kauli ya Dk Mwakyembe

Juzi, akitoa tamko baada ya kukerwa na kauli ya Jeshi la Polisi alisema mbunge huyo alisema ‘napata taabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matibabu yangu au walisoma taarifa “nyingine”, na kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au “walisomewa”!

"Nasema hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa waandishi wa habari, hakifanani kabisa na picha iliyoko kwenye taarifa halisi ya Hospitali ya Apollo inayotamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua, kukidhibiti au kukiondoa huku vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu: “hakulishwa sumu”, “hakulishwa sumu”

Dk Mwakyembe pia alitoa sababu kuu tatu za kupinga ripoti o ya DCI akisema:

"Kwanza, kwa kuingilia mchakato wa matibabu yangu na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake, unaoendelea katika Hospitali ya Apollo, nchini India, ambako bado sijahitimisha matibabu yangu, pili kwa ufinyu wa uelewa unaojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa “sikunyweshwa sumu” wakati sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu.

Alisema sababu ya tatu ni kitendo cha Jeshi la Polisi kujiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban mwaka mzima sasa, halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.

Dk Slaa

Akizungumzia sakata hilo, Dk Slaa alisema hana imani na ripoti ya uchunguzi iliyofanywa na Jeshi la Polisi na kutolewa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, kuhusu hali ya Mwakyembe.

"Mimi siwezi kuzungumzia ugonjwa wa mtu, lakini niseme tu kwa kifupi kuwa ripoti ya DCI Manumba siwezi kuiamini. Sina imani na Manumba kwa sababu mimi mwenyewe imenitokea,"alirusha kombora kwa Manumba.


"Niliwekewa vipaza sauti kwenye kitanda changu mjini Dodoma, taarifa za tukio hilo zilifika kwake lakini hadi leo hajatoa majibu yoyote ya uchunguzi wake," alisisitiza.

"Nani asiyemfahamu Manumba ndiye alishuhudia watu 50 wakipoteza maisha kwa kufukiwa mgodini na kesi ikaenda mahakamani, ikafutwa, Kwa nini Serikali yetu inamweka mtu wa aina hiyo kwenye nafasi kubwa kama hiyo," alihoji Dk Slaa.

Alisema hata katika tukio la kuwekewa vinasa sauti kwenye kitanda huko Dodoma, hakuwahi kuitwa na kuhojiwa.

Askofu Ruwa'ich
Akizungumzia mvutano huo, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Yuda Thadeus Ruwa'ichi, alisema kinachoendelea kati ya jeshi na Dk Mwakyembe, ni ishara ya kutosha kuwa taifa liko kwenye ubabaishaji.

"Malumbano hayo yanaonyesha kuwa taifa liko kwenye ubabaishaji na hiki siyo kitu kizuri. Ushauri wangu turudi na kuwa wakweli, tufanye kazi kwa uadilifu,"alisema askofu Ruwa'ichi.

Rais huyo wa TEC, pia aliwataka waandishi wa habari kufanya uchunguzi wao na kutoa taarifa za kubaini ukweli kuhusu jambo hilo, ili kuondoa utata uliopo.

Jukwaa la katiba

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba alielezea kushangazwa kwake juu ya nguvu aliyopata Manumba ya kupishana na mawaziri.
Alisema kinachotakiwa ni jopo la madaktari bingwa wa nchini, kuunda tume ili kuja na jibu litakalowawezesha wananchi waache kuihofia Serikali.

"Mabishano baina ya viongozi wa Kikwete (Rais), yanaonyesha dhahiri kwamba Serikali ina ulegevu, unaotokana na kiongozi wake mkuu kukaa kimya," alisema.
Kibamba alisema wakati umefika kwa Rais wa nchi kujitokeza hadharani na kuwawajibisha mawaziri, kama anaamini kuwa yanayoongelewa ni ya uwongo.
“Kilichoelezwa na Manumba hakiingii akilini kwa mwananchi wa kawaida, hii nchi sasa ni ya kisanii maana umegeuka mchezo wa Bongo land wa kuongea bila kuthitibishwa na madaktari bingwa,”alisema.

“Afya za mawaziri si suala la siri hasa ikizingatiwa kuwa wanatumia fedha za Watanzania katika kutibiwa . Kama kiongozi anataka kuweka siri aondoke kwenye uongozi atumie fedha zake,” alisisitiza.

“Siamini kama DCI Manumba ni daktari , kinachotakiwa ni kuundwa jopo la madaktari bingwa na Rais kuwaeleza Watanzania kinachowasibu viongozi wake,” aliongeza.

Alisema Watanzania wanaamini kuwa Dk Mwakyembe alilishwa sumu na kwamba ni vema Serikali ikaondoa mkanganyiko huo.


Akizumngumzia sakata hilo kwa njia ya simu, Mbunge wa Nyamagana, jijini Mwanza, Hezekiah Wenje alisema ni dhahiri kwamba kuna kitu ambacho Jeshi la Polisi linakificha.

“Hali halisi inaonyesha wazi kuwa kuna ukweli mwingi unaofichwa na Jeshi la Polisi na ndiyo maana kunakuwa na upotoshaji wa wazi,” alisema Wenje.

Mbunge huyo alisema kuna haja sasa ripoti ya madaktari kuwekwa wazi ili watu wajue.

Kwa upande wake, wakili wa kujitegemea mkoani Mwanza, Stephen Magoiga alisema Jeshi la Polisi, linaonyesha wazi kwamba lina matatizo makubwa ya kiutendaji linapotaka mlalamikaji kuwasilisha ushahidi.

Akikumbushia Dk Mwakyembe kudaiwa ushahidi alipopeleka malalamiko yake juu ya maisha yake kuwa hatarini, Magoiga alisema ushahidi ni suala la kitaalamu ambalo si mtu yoyote anaweza kukusanya.

“Jeshi la Polisi ndilo lenye utaalamu wa kukusanya ushahidi na wanalipwa kwa kazi hiyo, sasa wanapodai mlalamikaji alete ushahidi na baadaye kupingana na madai yake, ni dhahiri kwamba jeshi hilo linasema uwongo,” alisema Magoiga.

Alisema polisi wanapaswa kufanya kazi kisayansi kwa kuzingatia kwamba tuhuma za Dk Mwakyembe kulishwa sumu zimetolewa mara ya kwanza na mtu mzima mwenye hadhi yake katika jamii ya Kitanzania.

Alisema ni jambo la kushangaza kuona polisi wakioonyesha dharau za waziwazi kwa tuhuma zilizotolewa na mtu kama Waziri Samwel Sitta.

“Kama kauli ya Sitta inaweza kutendewa hivi na polisi je, ya mtu wa kawaida itakuwaje," aliohoji wakili huyo.


Ijumaa iliyopita Manumba alitoa tamko kuhusu kauli zilizowahi kutolewa na Sitta akiziita kuwa ni za uwongo na kuwataka watu wazipuuze.

Pia alitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Waziri huyo wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala, alisema mabishano yanayoendelea ndani ya Serikali, yanaonyesha kuwa kuna kitu kinachofichwa.
Profesa Mpangala alihoji kuhusu mahali ambako kumpa nguvu Manumba kuongelea afya ya Dk Mwakyembe.

Alisema kitendo hicho kinapingana na msimamo wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye aliwahi kukaririwa akisema Dk Mwakyembe ndiye anayepaswa kueleza hadharani maradhi yanayomsumbua.

Alisema Jeshi la Polisi limedharau kauli ya Pinda na kwamba hiyo inaonyesha kuwa Serikali, imekosa msemaji wa mwisho.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam
Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Musa Salim, alisema hatua ya viongozi kupishana inaonyesha kuwa hawafanyi kazi kwa umoja.

“Kilichoongelewa na Jeshi la Polisi ni sahihi kwa sababu limepewa jukumu la kuchunguza na kama kuna viongozi hao wanapinga majibu hayo, nadhani wanapaswa kuja na jibu,” alisema.

“Mimi sijui chochote lakini kama unachoeleza ni hivyo, maoni yangu ni kwamna tunatakiwa kuheshimu uchunguzi wa polisi ambao wamepewa dhamana ya kuchunguza,” alisema Sheikh Salim.


Historia ya ugonjwawa Mwakyembe
Dk Mwakymbe alianza kuumwa Oktoba 9 mwaka jana na baadaye kupelekwa India ambako alilazwa katika Hospitali ya Apollo kwa matatibu.

Alirejea nchini Desemba 11 mwaka jana, baada ya kulazwa hospitalini kwa takribani miezi miwili.


Msemaji wa familia ya Dk Mwekyembe ambaye ni Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa alisema mara baada ya mbunge huyo wa Kyela kuwasili nchini kuwa, afya yake ni nzuri na ndio maana ameruhusiwa kutoka hospitalini.

Kauli za Waziri Sitta

Mara kadhaa Waziri Sitta amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari akisisitiza kuwa ugonjwa wa Dk Mwakyembe, umetokana na kulishwa sumu.

Akiwa kwenye uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima kutoka kwa kiongozi, iliyoanzishwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe, Jijini Dar es Salaam Januari 28 mwaka huu, Sitta alisema “ Dk Mwakyembe kapewa sumu, kama vyombo vya uchunguzi vinasema siyo, basi watueleze ukweli, tena haraka.”

“Ni vipi uone binadamu ambaye ukimshika katika ngozi unga unamwagika chini, mhudumu anakuja kuufagia, lakini baada ya saa moja unarudia tena, kitu hicho si cha kawaida,” alisisitiza Sitta.

Sitta alisema wamejaribu wameshindwa kwa kuwa Dk Mwakyembe analindwa kwa jina la Yesu ambalo ni kubwa kuliko yote.

Waziri Nahodha

Hata hivyo, akijibu moja ya kauli hizo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nohodha alimtaka Waziri Sitta awasilishe ushahidi wake ili ufanyiwe kazi badala ya kuzungumza nje ya vyombo vya sheria.

Lakini, Sitta alisema hatapeleka ushahidi kuhusu madai kwamba Dk Mwakyembe alilishwa sumu kwa kuwa polisi tayari wana ushahidi.

Alilaumu kuwa hata yeye aliwahi kupeleka tuhuma za kutaka kuawa lakini alipuuzwa.



Alisema inachotakiwa kufanywa na polisi ni uchunguzi kuhusu madai ya Dk Mwakyembe kulishwa sumu.

“Waziri Nahodha anataka ushahidi gani ikiwa taarifa za madaktari zinazomhusu Dk Mwakyembe kuhusu sumu aliyopewa zilishapelekwa polisi, anataka mimi nitoe ushahidi gani,” alisema Waziri Sitta. Chanzo,Gazeti la Mwananchi

No comments:

Powered by Blogger.