WAZIRI MAKAMBA ASISITIZA MATUMIZI YA MAJIKO BANIFU KATIKA UKAUSHAJI WA TUMBAKU
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January
Makamba akifafanua jambo kuhusu wananchi waliovamia msitu wa hifadhi ya
Kijiji. Kushoto ni Bi. Veronica Nyasa mkazi wa eneo hilo ambae amesema
yuko tayari kuondoka endapo atapatiwa sehemu mbadala.
Uongozi
wa Wilaya ya Kaliua wakimwonyesha Waziri Makamba magogo ya miti ya
asili yanayotumiwa na wanachi katika kukaushia tumbaku kwa kutumia
majiko ya kienyeji
Pichani
ni moja ya majiko ya kienyeji yanayotumia kuni/miti mingi katika
kukaushia tumbaku. Waziri Makamba amewaagiza wakazi wa Kitongoji cha
Mtakuja Magharibi kutumia majiko banifu ili kunusuru ukataji miti kwa
wingi husnan ile ya asili
…………………………………………………………………
Na Lulu Mussa-Tabora
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira hii leo
ameendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa wa Tabora akitokea Mkoani
Kigoma.
Akiwa
Mkoani Tabora Waziri Makamba ametembelea Wilaya ya Kaliua na kukutana na
changamoto kubwa ya Uharibifu wa Mazingira na Uvamizi wa Misitu
unaofanywa na wananchi. Katika Kijiji cha Ufugala Wilaya ya Kaliua
Waziri Makamba amefanya Mkutano wa hadhara kijijini hapo na kubaini kuwa
Kitongoji hicho hakikufuata taratibu za kisheria katika kuanzishwa
kwake na kimeanzishwa ndani ya Hifadhi.
Akitoa
maelezo ya Awali Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Bw. Abel Yeji Busalama
amemueleza Waziri kuwa Kitongoji hicho kiko ndani ya Hifadhi ya Msitu wa
Kijiji ambapo jumla ya Vijiji 11 viamua kutenga eneo hilo kwa ajili ya
Hifadhi.
Bw. Busalama amesema kuwa wakazi hao wamekwisha amriwa kuondoka katika hifadhi hiyo na utekelezaji wake unaendelea.
Akijibu
hoja zilizowasilishwa na wakazi wa eneo hilo Waziri Makamba amesema
kuwa wajibu wa Serikali ni kuhakikisha kuwa Sheria, tararibu na kanuni
zinafuatwa bila kukiukwa. Waziri Makamba pia amesisitiza kuwa maamuzi ya
matumizi bora ya ardhi yapo mikononi mwao. “Ndugu zangu ni nyinyi
wenyewe mliamua kutenga eneo hili maalumu kwa hifadhi ya msitu wa kijiji
na kufuata taratibu zote za kisheri katika kuusajili, maamuzi yenu ya
awali yatabaki palepale mpaka mtakapofuata taratibu nyinginezo.” Makamba
alisisitiza.
Aidha,
Waziri Makamba ameahidi kuwasilisha suala hilo kwa Wizara ya Maliasili
na Utalii na ile ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kupata
ufumbuzi wa kudumu. “Nitaongea na Mawaziri wenzangu na kuleta timu ya
wataalumu kupitia upya mipaka ya kijiji na kuifanyia kazi” Makamba
alisisitiza.
Kuhusu
hifadhi ya Mazingira Waziri Makamba amewataka wakazi wa Ufulaga kuacha
tabia ya kukata miti ya asili na kusisitiza kuwa uharibifu wa mazingira
unabadilisha tabia za watu. “Wana Ufulaga, binadamu wakiharibu mazingira
kwa kiasi kikubwa wanaanza wizi na udokozi na wanyama wataanza kuwinda
watu kwa kukosa malisho” alisema Waziri Makamba.
Waziri
Makamba pia amefanya ziara katika Wilaya ya Urambo na kubaini
changamoto kubwa ya uvamizi wa misitu na ukataji wa miti ya asili kwa
ajili ya kuni za kukaushia tumbaku.
Waziri
ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)
kutumia Sheria ya Mazingira namba 20 ya mwaka 2004 kifungu namba 196 (1)
(a na b) kupiga marufuku ya matumizi ya majiko banifu ya kienyeji pia
ukataji mkubwa wa miti ya asili kwa ajili ya biashara ya tumbaku. Katazo
hilo litawahusu Wakulima na Vyama vya Msingi vyote vinavyojishughulisha
na biashara ya tumbaku.
Waziri Makamba anaendelea na ziara yake kwa kutembelea Wilaya za Nzega na Igunga.
No comments:
Post a Comment