TPDC YAWANOA WAANDISHI WA HABARI.
Mkurugenzi
Mtendaji wa TPDC, Dkt James Mataragio akiongea na waandishi wa habari
wakati wa warsha iliyofanyika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
Mkurugenzi
wa shughuli za mkondo wa juu (Upstream Operations) kutoka TPDC, Ndugu
Kelvin Komba akitoa mada wakati wa warsha ya waandishi wa habari
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Said Meck Sadick akiwa katika picha ya
pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio na
Wakurugenzi wengine kutoka TPDC pamoja na waandishi wa habari.
SEKTA
ya gesi na mafuta imeendelea kukua kwa kasi nchini kwetu, ukuaji wa
sekta hii unakuja na fursa na changamoto zake. Mojawapo ya changamoto
kubwa ni uelewa wa sekta hii kwa wananchi na mategemeo makubwa yaliyopo
miongoni mwao. Katika kulitatua hili, Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) limeendesha semina ya siku mbili jijini Dar es Salaam
ikiwa na lengo la kutoa elimu ya mafuta na gesi kwa waandishi wa habari
ili kuwajengea uwezo zaidi wa kuupasha habari umma. Mgeni rasmi katika
warsha hiyo alikua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Said Meck
Sadick.
Akiongea
wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dr.
James Mataragio alisema “ warsha hii inalenga kuendelea kuwajengea uwezo
zaidi waandishi wetu wa habari kuweza kuripoti kwa umahiri na ustadi
habari za mafuta na gesi”. Dr. Mataragio aliwashukuru waandishi wa
habari kwa juhudi zao za kuupasha habari umma na kuwaasa kwamba kalamu
yao ina nguvu hivyo ni vyema ikaendelea kutumika kujenga uchumi wa Taifa
kwa kutoa taarifa sahihi kila wakati.
Katika
taarifa yake Mkurugenzi Mtendaji alisisitiza juu ya matarajio yasiyo
halisia yaliyopo miongoni mwa wanajamii na kuwaomba waandishi wa habari
kusaidia kuwaeleza wananchi juu ya uhalisia wa sekta. Dr. Mataragio
alisema kwamba uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi ni wa gharama
kubwa na hata mafaniko kwa maana ya mapato makubwa kwa Serikali huchukua
muda mrefu kuonekana.
Akitolea
mfano mradi mkubwa wa kusindika gesi asilia (Liqufied Natural Gas-LNG),
Dr. Mataragio alifafanua kwamba itachukua takribani miaka 8 hadi 10
kabla ya mzigo wa kwanza wa LNG kusafirishwa kwenda katika soko la dunia
kwa mauzo. Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC alisisitiza juu ya
ushiriki wa wazawa katika sekta hii hususan katika kutoa huduma na kuuza
bidhaa. Sheria mpya ya petroli ya mwaka 2015 inawataka wawekezaji wote
kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na kama ikitokea bidhaa hizo
hazipo nchini basi kampuni iingie ubia na kampuni ya kizawa ili kuweza
kutoa huduma inayohitajika. Sheria imeeleza kwamba ubia huo lazima umpe
mzawa ushiriki usiopunguza asilimia 25%, hii ni fursa kwa wazawa na ni
vyema ikachangamkiwa.
Nae mgeni rasmi wa warsha hiyo, Ndugu Said Meck Sadick, Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam alisisitiza juu ya umuhimu wa kulinda miundombinu
ya Taifa kwa kuwa ni mali yetu wananchi wa Tanzania hivyo jukumu la
ulinzi ni letu sote. Mkuu wa Mkoa aliyasema haya akilenga ulinzi
shirikishi katika miundombinu ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia
ambayo imejengwa na TPDC kwa mkopo kutoka EXIM Bank ya China na
kudhaminiwa na Serikali ya Tanzania. Ndugu Said Meck Sadik alisisitiza
vile vile juu ya utoaji taarifa mapema pale mtu anapoona kuna hujuma au
uharibifu wa aina yoyote katika miundombinu hii, akiongea katika warsha
hiyo alisema “miundombinu hii ya gesi na mafuta ni mali ya watanzania
hivyo kuilinda ni jukumu letu sote kama wazalendo wa nchii hii”.
TPDC imeendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ikiwa na lengo la
kuongeza uelewa zaidi katika sekta hii mpya na changa ya mafuta na gesi
hapa nchini.
No comments:
Post a Comment