WATANZANIA WATAKIWA KUTODANGANYWA KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA

Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dodoma.
MJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba ambaye pia ni
Mwenyekiti wa TCD Mhe. John Cheyo amewataka Watanzania kutodanganywa kuhusiana
na mchakato mzima wa kusaka Katiba Mpya.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mhe. Cheyo wakati
alipokuwa akifanya mahojiano katika kipindi cha asubuhi cha Jambo kinachorushwa
na Televisheni ya Shirika la Habari Tanzania (TBC).
Mhe. Cheyo amesema kuwa ni vema viongozi kuacha kusema
uwogo na kuwa waungwana katika mchakato wa kutafuta Katiba Mpya kwani si vema
kuitakia Tanzania mabaya bali ni kutaka mchakato huo wa Katiba uendelee kwa
amani.
Ameongeza kuwa Taifa la Tanzania linahitaji kuwa Taifa
lenye nguvu kwani amani haiwezu kuwekewa thamani kwa vurugu, hivyo ametaka
amani iliyopo nchini ilindwe na kuepuka kudanganywa na baadhi ya watu wasiokuwa
na nia njema na nchi.
Mhe. Cheyo ameshangazwa kwa kitendo cha viongozi wa
UKAWA kutoweka ajenda ya kurudi ndani ya Bunge hilo wala kuzungumzia kuhusu suala
hilo la kurudi ndani, bali wamekuwa wakitaka wajumbe wengine walioko ndani
watoke kwa kusema kuwa bunge hilo sio halali.
“Nawashangaa UKAWA kwa kutoweka ajenda ya kurudi ndani
ya Bunge hili Maalum la Katiba na badala yake wao wanaweka ajenda ya kutoka ndani
ya bunge hili tena kwa nguvu”, alisema Mhe. Cheyo.
Aidha, Mhe. Cheyo amewataka vijana nchini wawe na
mshikamano na kuepuka kudanganywa na viongozi kwa kuambiwa mambo yenye uwongo
huku akisisitiza kuwa Rais aliyeko sasa hivi ana nia njema ya kuipatia nchi
Katiba iliyo bora na yenye kumfaa kila Mtanzania.
No comments:
Post a Comment