Header Ads

MATOKEO YA KIDATO CHA SITA 2014 IWAWA SEKONDARI, MKUU WA WILAYA YA MAKETE ATOA WOSIA

Na Edwin Moshi, Makete

Walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Iwawa iliyopo Makete mkoani Njombe wametakiwa kutoridhika na kubweteka na shule hiyo kushika nafasi ya nne kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita 2014 yaliyotangazwa miezi michache iliyopita

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro katika hafla ya kuwapongeza walimu wa Iwawa sekondari baada ya shule hiyo kushika nafasi ya 4 kitaifa, nafasi ya 2 kikanda na nafasi ya 1 kwa mkoa wa Njombe katika matokeo ya kidato cha sita mwaka huu

Amewapongeza walimu kwa jitihada zao za kufundisha pamoja na moyo wa wanafunzi katika kujisomea ambavyo kwa pamoja vimepelekea kuitangaza wilaya ya Makete kielimu na kuwataka kupanda na kushika nafasi za juu katika mitihani inayofuata
"Ni kweli mnastahili pongezi lakini nawaombeni ongezeni bidii ili mitihani inayokuja mwakani mpande zaidi ya hapa, muitangaze wilaya yetu, tukishirikina pamoja tunaweza" amesema Matiro

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya amewataka wananchi kushirikiana katika kuchangia maendeleo ya shule kwani serikali inaunga mkono jitihada zao pale tu inapoona wamechangia

Amesema kumekuwa na kasumba ya watu wachache kuwakatisha tamaa wananchi wengi wenye moyo wakuchangia miradi ya shule, na kusema wananchi wasikatishwe tamaa na watu wa aina hiyo kwani serikali haiwaachii peke yao, wao wakichangia kwa kiasi fulani serikali nayo humalizia palipobakia huku akisisitiza kuwa kwa shule zenye upungufu wa walimu, serikali inalitambua tatizo hilo na ndiyo maana inapanga walimu wapya kila mwaka katika shule hizo na mwishowe upungufu huo utamalizika

Awali akisoma taarifa ya shule kwa mkuu wa wilaya, mkuu wa shule hiyo Mwl. Antony Ng'wavi amesema shule yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa pamoja na walimu jambo ambalo linachangia kupungua kasi ya ufaulu kwa kiasi kikubwa zaidi, huku akiahidi kuwa mwakani shule yake itafanya vizuri kuliko mwaka huu

No comments:

Powered by Blogger.