Bodi ya mikopo yatangaza kuanza kupokea maombi
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Bw. Cosmas Mwaisobwa akisisitiza
jambo mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam alipokua
akitangaza kuhusu kuanza kupokea maombi ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo
vikuu kuanzia 1 Mei, 2013.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu imetangaza kuanza kupokea maombi ya mikopo kwa wafunzi
wanaotarajiwa kujiunga na Vyuo Vikuu pamoja na wanafunzi wanaoendelea
kwa mwaka wa masomo 2013/2014 kuanzia Mei 1, 2013.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Bodi
hiyo Bw. Cosmas Mwaisobwa amewaambia waandishi wa habari jana jijini Dar
es Salaam kuwa maombi ya mikopo yatafanyika kwa njia ya mtandao kupitia
anuani ya http://olas.heslb.go.tz.
Amesema vipeperushi maalum vyenye
maelezo ya jinsi ya kuomba mkopo kwa njia ya mtandao vinapatikana kwenye
Vyuo vya Elimu ya Juu, ofisi za Elimu za Wilaya,watoa huduma ya
Intaneti, Makao Makuu ya Bodi ya Mikopo na Ofisi za Bodi ya Mikopo za
Kanda.
Pia alisema maelezo haya ya mikopo yanapatikana kwenye tovuti ya bodi ambayo ni: www.heslb.go.tz.
Waombaji wapya wanatakiwa kulipa
ada ya maombi ya mikopo ya shilingi 30,000/- huku wanafunzi walio katika
mwaka wa masomo wa tano au wa sita wa masomo wataendelea kulipa ada ya
maombi ya shilingi 10,000/-.
"Wanafunzi wa mwaka wa pili, tatu
na nne ambao walilipa ada ya maombi ya shilingi 30,000/- katika miaka ya
masomo ya 2009/2010, 2010/2011 na 2011/2012 hawatakiwi kulipa tena ada
hiyo ya maombi ya mikopo," alisema.
Bwana Mwaisobwa amesema mwombaji
wa mkopo huo anapaswa kuwa na sifa ambazo zimetajwa katika kifungu cha
17 cha Sheria Na 9 ya mwaka 2004 ambazo ni pamoja na na mwombaji kuwa
raia wa Tanzania.
Ametaja sifa nyingine kuwa ni
kudahiliwa katika chuo cha elimu ya juu, kutokuwa na njia nyingine ya
kugharamia elimu ya juu, kufaulu mitihani ya mwaka uliotangulia kwa
waombaji wanaoendelea na masomo pamoja na kuwa mhitaji.
"Bodi inasisitiza kwamba waombaji
wa mikopo wazingatie muda uliopangwa na pia kufuata kwa umakini taratibu
zote zilizoainishwa katika uombaji wa mikopo," alisema na kusisitiza
kuwa hakutakuwa na muda wa ziada baada ya muda uliopangwa kupita.
Mwisho wa kupokea maombi hayo ya mikopo ni 30 Juni 2013.
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu kwa mwaka wa masomo wa 2012/2013 iliwapatia mikopo wanafunzi wapatao 94,703.
No comments:
Post a Comment